NA JOSEA SINKALA, MBEYA.
Jeshi la Zimamoto na Uokozi Mkoa wa Mbeya kupitia maonesho ya kimataifa ya wakulima (Nanenane) linatoa elimu ya Zimamoto kwa njia mbalimbali ikiwemo kutumia farasi kuitangaza namba ya dharura ya 114 yanapotokea majanga mbalimbali.
Afisa habari kutoka Jeshi la Zimamoto na Uokozi Mkoa wa Mbeya Esther Kinyaga ndiye amekuwa akiongoza dawati la utoaji elimu hiyo kwa wahudhuriaji mbalimbali wa Nanenane ndani ya uwanja wa John Mwakangale jijini Mbeya akitumia mbinu hiyo kuyafikia mabanda mengi zaidi ya maonesho.
Mbali na kutumia farasi, Jeshi la Zimamoto na Uokozi Mbeya limekuwa likitumia mbinu mbalimbali kuwafikia wananchi kwa kufanya mikutano kwenye masoko, maegesho ya malori, vituo vya mabasi katika Wilaya zote za Mkoa wa Mbeya sanjari na kupitia vyombo vya habari.
Mbinu hizo zimeelezwa na Jeshi hilo kupunguza matumizi mabaya ya namba 114 ambapo baadhi ya wananchi walikuwa wakitumia kutoa taarifa za uongo kuhusu matukio ya moto ambapo Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mara nyingi limekuwa likifika eneo husika na kukuta taarifa si za kweli hivyo wananchi wanaaswa kutumia namba hiyo vizuri ili kuokoa majanga mbalimbali ikiwemo ya moto.