Home KITAIFA WIZARA YA MAENDELEO YA JAMII, FEDHA KUSHIRIKIANA KUELIMISHA JAMII

WIZARA YA MAENDELEO YA JAMII, FEDHA KUSHIRIKIANA KUELIMISHA JAMII

Na WMJJWM, DODOMA

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi maalum inajipanga kutoa elimu ya masuala ya fedha kwa jamii hasa makundi maalum kwa kushirikiana na Wizara ya fedha na Mipango.

Hayo yamebainika kwenye mafunzo yaliyotolewa na Wataalamu kutoka Wizara ya Fedha na Mipango kwa Menejimenti na watumishi wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, kuhusu fursa zinazopatikana katika masuala ya fedha, leo Juni 30, 2023 jijini Dodoma.

Akifungua Mafunzo hayo, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt Dorothy Gwajima, amesema ushahidi unaonesha kuwa, yapo Makundi mengi ndani ya Jamii ambayo yanatamani kuchangamkia fursa za kiuchumi lakini wanashindwa kutokana na kutokuwa na taarifa ya wapi pakuanzia.

Amesema Wizara itashirikiana kwa karibu zaidi na Wizara ya Fedha na Mipango kutoa elimu ya fedha kwa wataalamu ili wakaielimishe jamii hadi ngazi ya chini.

“Mwaka 2022 nilipata Bahati ya kutembelea Maonesho ya Saba Saba na kupita kwenye taasisi kadhaa za fedha ambapo nilibaini uwepo wa fursa ambazo wanajamii wengi hawazifahamu” amesema Waziri Dkt. Gwajima.

Aidha Waziri Dkt. Gwajima amesema mafunzo hayo yanasaidia kubadili fikra kuanzia ngazi ya watendaji ili wawe daraja imara kuwafikia wananchi kwa taarifa sahihi hasa wanawake na makundi maalum ndani ya jamii.

Kwa upande wake Kamishna wa sekta ya Fedha kutoka Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Charles Mwamwaja amesema Jamii ina kila sababu ya kuelimishwa kuhusu fursa na matumizi ya fedha katika maisha yao ya kila siku na kubadili utaratibu wa nidhamu ya fedha kwa kuwa na utaratibu wa kuweka akiba.

Dkt. Mwamwaja amebainisha kuwa, tafiti nyingi zilizofanyika zinaonesha watu wengi hawana uelewa mpana wa fursa zilizopo katika Sekta ya fedha, hivyo kupitia Wizara fedha wameendelea kutoa Elimu hiyo kwenye Jamii.

“Uwekaji wa akiba ni suala la Msingi sana, unapoona miradi mikubwa inafanyika leo hii, ni kwa kuwa tunajua tukishaweka miundombinu hii inachangia sana ukuaji wa uchumi, barabara, maji, umeme nk. vinapofika lazima Thamani ya eneo hilo inakuwa juu zaidi.” Amesema Dkt. Mwamwaja.

Naye Mtaalam wa fedha Bi. Dionisia Mjema, anayesimamia huduma ndogondogo za Kifedha kutoka Wizara ya Fedha, ameelezea mkakati wa Programu ya Elimu ya fedha kwa Umma pamoja na kusisitiza suala la uwekezaji kwenye Masoko ya hisa.

Previous articleWAZIRI BASHE AWEKA WAZI MPANGO WA WIZARA YA KILIMO KUIFANYA WILAYA YA MAKETE KUWA YA MFANO KWENYE KILIMO CHA NGANO
Next articleTPA YAWASILISHA MAPENDEKEZO YA MABORESHO YA TOZO MPYA ZA BANDARI NCHINI

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here