Wenyeviti wa vitongoji watatu pamoja na wajumbe saba wa Serikali ya kijiji cha Uhambule halmashauri ya wilaya ya Wanging’ombe mkoani Njombe wamejiuzulu nyadhifa zao kwa madai ya kuwa ni kutokana na serikali kushindwa kupeleka nishati ya umeme kwenye maeneo yao.
Miongoni mwa vitongoji ambavyo wenyeviti wake wamejiuzulu ni pamoja na kitongoji cha Fwimi,Masasati na Igominyi,wote wakidai sababu kubwa ni kutokana na kutotekelezeka kwa ahadi ya kupelekewa umeme licha ya kuahidiwa kwa muda mrefu.
Mkuu wa wilaya ya Wanging’ombe Claudia Kitta amewataka viongozi hao kurejea kwenye nafasi zao na kuendelea kuwatumikia wananchi kwa kuwa serikali inaendelea kutoa huduma hiyo na imekusudia kufikisha umeme kwenye kila kitongoji.
“Hili linatusikitisha lakini mpango wa Serikali ulianza kwa awamu na upande wa vitongoji tayari Serikali imeana kutekeleza maana vijiji vyote 108 vinavyohudumiwa na wilaya vimepata umeme na wanaendelea kutawanya kwenye vitongoji,Sasa kama unazila kazi unamuachia nani kwa hiyo niombe viongozi hawa ikiwezekana warudi kwa kuwa wameaminiwa na wenzao waweze kuwatumikia”Amesema Claudia Kitta DC wa Wanging’ombe.