Home KITAIFA WENYE MASHAKA AU WASIWASI NA DIRA (MITA) ZA MAJI WAENDE WAKALA WA...

WENYE MASHAKA AU WASIWASI NA DIRA (MITA) ZA MAJI WAENDE WAKALA WA VIPIMO (WMA) KWA UHAKIKI

Wenye mashaka au wasiwasi na dira (mita) yake ya maji anakaribishwa kituo cha uhakiki wa Vipimo Misugusugu kuhakiki dira hiyo ili ajiridhishe iwapo kiasi cha maji anachopata kinawiana na ankara ya maji anayolipa fedha.

Wito huo umetolewa na Meneja wa Wakala wa Vipimo kituo cha uhakiki Vipimo Misugusugu Bwana Charles Mavunde Ofisini kwake Misugusugu Kibaha mkoani Pwani wakati akizungumza na Waandishi wa habari akiwakaribisha wananchi wenye changamoto mbalimbali za matumizi ya dira (mita) na wasambazaji na wauzaji pia wa dira maji kwa Mamlaka za maji nchini.

Amesema kuhakiki dira za maji ni moja ya jukumu la Wakala wa Vipimo (WMA) nchini lengo likiwa ni mwananchi aweze kupata maji na kulipa ankara ya maji kwa usahihi kulingana na huduma ya maji aliyopata kupitia dira anayotumia.

Amesema Wakala wa Vipimo (WMA) Tanzania na Kituo cha Misugusugu wamepewa jukumu hilo na serikali kwa mujibu wa sheria ya Vipimo sura 340 pia kwa utekelezaji wa ilani ya uchaguzi mkuu ya CCM ya mwaka 2020. Sheria ya Vipimo inawataka wasambazaji wa dira za maji na mamlaka za maji kabla hawajamfungia mteja dira kuhakikisha imehakikiwa ili apate huduma ya maji kwa usahihi hivyo ni lazima dira za maji zipelekwe kwa Wakala hao wa Vipimo kuhakikiwa na baada ya kuhakikiwa ifungwe rakiri ya serikali na ndipo mwananchi afungiwe dira hiyo.

“Nitoe wito kwa wananchi, Mamlaka za maji na vikundi vya watumia maji wenye wasiwasi wowote, wanataka kuuliza lolote dira za maji mnakaribishwa kwenye Kituo chetu Misugusugu ili kituo kwa kushirikiana na Mamlaka za maji kutatua changamoto hiyo inayohusu dira za maji ili mwananchi atumie dira hiyo kwa usahihi na apate faida katika matumizi ya maji lakini pia Mamlaka za maji ziweze kutoa huduma nzuri kwa Wananchi”

Mavunde amesema faida wanayopata Mamlaka za maji zinazohakiki dira zake ni kutoa kiasi halisi cha uniti sahihi za mtumiaji wa maji ili alipie kwa usahihi sawa na kiasi cha maji alichotumia.

“Ili Mamlaka za maji ziweze kupata kiasi halisi cha maji kilichosambazwa kwa Wananchi lazima dira za maji zihakikiwe kwa usahihi na Wakala wa Vipimo (WMA) ili Wananchi waweze kupata ankara sahihi na Wananchi waweze kulipa ankara hizo sawa na matumizi yao”

“Kama dira za maji hizo zina changamoto zozote za kuzidisha, kupunja au kuvuja au zina tatizo la kimetrolojia matatizo hayo hubainika wakati wa uhakiki hivyo dira za maji aina hiyo haziwezi kuruhusiwa kutumika.

“Tunahakiki dira za maji mpya na zilizo majumbani kwenye matumizi zenye vipenyo vidogo na zile zenye vipenyo vikubwa kwaajili ya utoaji wa huduma za maji nchini”

Amesema dira hizo kufikia kwenda kufungwa kwa mtumiaji lazima zitahakikiwa kwa usahihi ili kuona kama zinafaa bila kumwibia wala kumpunja mtumiaji wa dira hizo za maji.

“Dira za maji zaidi ya laki tatu zimekwisha hakikiwa katika Kituo hiki cha Wakala wa Vipimo cha Misugusugu tangu mwaka 2019 kilipoanzishwa na kwa mujibu wa mitambo iliyopo Misugusugu mita 1800 zinaweza kuhakikiwa kwa siku ” amesema Mavunde.

Aidha Mavunde amezitaka Mamlaka za maji nchini, wauzaji wa dira za maji kuzingatia utekelezaji wa sheria ya Vipimo sura 340 kwa kupeleka dira zao kupeleka kuhakikiwa kabla ya kufungwa kwa mtumiaji.

Previous articleKUCHELEWESHWA KWA FEDHA YA KUJIKIMU KWAPUNGUZA ARI YA UTENDAJIKAZI HALMASHAURI YA WILAYA MOROGORO
Next articleJESHI LA UHAMIAJI MWANZA WAPATA TUZO YA UTOAJI HUDUMA BORA KATIKA MAONESHO YA AFRIKA MASHARIKI

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here