KATIBU Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia ,Wanawake na makundi maalum dkt. John Jingu amewataka wadau wanaohusika na kufanya utafiti wa ukatili dhidi ya watoto (VACS) 2024 kuzingatia weledi ili kubaini ukubwa wa tatizo na namna ya kukabiliana nalo.
Akifungua kikao cha wadau cha kujadiliana nakukubaliana mikakati ya utafiti wa kitaifa wa masuala ya ukatili dhidi ya watoto kilichofanyika Julai 19, 2023 jijini Dodoma dkt. Jingu amesema kwakuwa utafiti ni nyenzo muhimu ya kupambana na ukatili dhidi ya watoto ni wajibu kwa kila mdau kufanya kwakufuata maadili .
‘’Huwezi kuchukua hatua zozote zile na ukafanikiwa kama adui humjui vizuri, sasa utakuwa unapigana ngumi kwenye giza, kumbe utafiti huu ni nyezo muhimu sana ya mapambano dhidi ya ukatili,’’amesema Dkt. Jingu.
Dkt. Jingu amesema ipo haja ya kufanya utafiti huo ambao utasaidia kupata taarifa sahihi zitakazowezesha kupambana na ukatili dhidi ya watoto kwakuwa ni rasilimali muhimu katika taifa.
‘’Bahati nzuri Serikali yetu inathamini sana utafiti, mwaka jana kama taifa tumetoka kufanya utafiti mkubwa sana tunaita sensa na kwa mafanikio ili kupata takwimu zinazotusaidia kufanya maendeleo kama taifa na saivi tumejipanga kwenye kufanya utafiti siyo mkubwa ili utatusaidia kupata taarifa sahihi kwaajili ya kushughulikia changamoto ya ukatili dhidi ya watoto,’’.
Amewataka kufanya utafiti kwa weledi unaohitajika na kwa njia zinazokubalika na kuongeza kuwa mbinu zitakazotumika ziwe sahihi nazitakazosaidia kupata taarifa sahihi na ziendane na mazingira ya jamii yetu.
Amefafanua kuwa kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinasema kwa mwaka 2022 jumla ya watoto Bilioni 1 walifanyiwa ukatili , huku asilimia 50 ya watoto katika bara la Afrika walifanyiwa kitendo hicho.
Kwa upande wa Mkurugenzi Msaidizi huduma za ustawi wa jamii kutoka OR-TAMISEMI, Bi.Subisya Kabuje, amewataka Wadau wanaotekeleza utafiti huo kuhakikisha wanaweka usiri wa mahojiano yao na watoto na kuwatumia Wataalamu wakati wakitekeleza Zoezi hilo ili kuwasaidia watoto waliofanyiwa ukatili kuwa sawa Kisaikolojia.
Naye Meneja wa Methodolojia za Takwimu na uratibu kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Bw.Emilian Karugendo amesema moja ya nguzo katika kukusanya taarifa ya Mtu mmoja mmoja ni usiri hivyo hazitakiwi kutoka Kwa namna yeyote Ile.
Pia ametoa wito Kwa wadau kuhakikisha wanatumia Takwimu hizo Kwa malengo yaliyokusudia Huku akiahidi kuwa ofisi ya Takwimu Tanzania na Visiwani ipo tayari kutoa ushirikiano wowote Kwa wadau kadiri watakavyouhitaji.
Mkurugenzi wa Shirika la THPS Dkt.Redempta Mbaya amesema katika Mkutano huo watapata nafasi ya kujadiliana ukubwa wa utafiti,umuhimu wa utafiti na majukumu ya Kila Mdau katika kutekeleza utafiti wenyewe hivyo baada ya utafiti huo watajua ukubwa wa tatizo Kwa wanaamini matukio yanayoripotiwa ni machache kuliko Yale ambayo hayaripotiwi.