Waziri Mkuu Kasimu Majaliwa Julai 7, 2023 ameendelea na ziara yake ya kikazi katika Mkoa wa Mtwara na amekagua ujenzi wa miundombinu na vifaa tiba katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Ligula zilizopo Mkoani Mtwara.
Majaliwa amesema kuwa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan inataka kuona wananchi wakipatiwa huduma za afya popote walipo ili kuepuka kuzifuata maeneo ya mbali.
“Tumejenga vituo vya afya, hospitali za wilaya na sasa tunajenga hospitali kwenye kila Halmashauri ili kusogeza huduma zaidi kwa wananchi, nia ya Serikali ya awamu ya sita ni kuona wananchi wetu wanapata huduma muhimu hukohuko waliko,” Majaliwa amesema.
Akizungumza na watumishi wa Hospitali ya Kanda ya Kusini amesema malengo ya Rais Samia Suluhu ni kuifanya Hospital hiyo iwe mkombozi kwa wana Kusini na Nchi jirani za Comoro na Msumbiji.
Aidha Rais Samia Ameongeza fedha kwenye bajeti ya Wizara ya Afya kwaajili ya uboreshaji wa miundombinu na vifaa tiba vya kisasa kwenye maeneo yote ya utoaji wa huduma za afya.