NA JOSEA SINKALA, MBEYA.
Jumuiya ya Wazazi wa CCM Wilaya ya Mbeya vijijini (kichama) chini ya Mwenyekiti wake William Simwali, imeshauri mpango wa uwekezaji wa Bandari kurudi ndani ya Chama (CCM) kuanzia ngazi ya Taifa, Mikoa, Wilaya hadi mashina ili kuwa na uelewa wa pamoja katika kuwashauri wananchi juu ya umuhimu wa uwekezaji huo badala ya kuwa na majibu yanayokinzana.
Simwali amesema uwekezaji ni muhimu lakini baadhi ya viongozi wa Chama hicho na Serikali kila mmoja amekuwa na majibu yake kuhusu bandari wakijibu hoja za wanaopinga uwekezaji huo wakiwemo wapinzani.
“Suala la Bandari ni uchungu kwa sisi CCM. Ni muhimu suala hili lingejadiliwa kwa kina kwenye vikao vya ndani ya Chama ngazi zote kama ilivyofanyika kwenye NEC Taifa kuliko kuanza na mikutano ya hadhara”, Ameshauri Simwali.
Amesema ni vizuri wana CCM wakakaa chini kupitia mikutano mikuu ya Mikoa hadi Wilaya ili kujua ukweli ndipo watoke nje ili kusaidia kuwa na maelezo yanayofanana kote nchini sanjari na kuwa na majibu ya maswali yanaulizwa na wafuatiliaji mbalimbali.
“Hivi mwana-CCM anaweza kunyosha mkono na kuumuuliza Katibu mkuu Taifa swali kwenye mkutano wa hadhara ambalo linaweza kukiumiza chama? Yatupasa kukaa na kutafakari kwa kina”, amehoji na kueleza Mwenyekiti huyo wa Jumuiya ya Wazazi Wilayani Mbeya vijijini.