Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Mohamed O. Mchengerwa amemuelekeza Katibu Mkuu OR-TAMISEMI kuwachukulia hatua za kinidhamu watumishi 7 wa Halmashauri ya Wilaya ya Liwale Mkoani Lindi kwa kushindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo hivyo kuzorotesha utendaji kazi wa shughuli mbalimbali za Halmashauri hiyo.
Mhe. Mchengewa amechukua uamuzi huo wakati wa ziara katika Wilaya ya Liwale ya kukagua na kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Waziri Mchengerwa ameelekeza hatua za kinidhamu zichukuliwe kwa mujibu wa Kanuni ya 42 ya Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2022 inayoainisha kuwashusha vyeo, kukatwa mshahara kwa asilimia 15 kwa muda usiopungua miaka 3 pamoja na kufukuzwa kazi iwapo watabainika kufanya makosa hayo.
Watumishi wanaotakiwa kuchukuliwa hatua hizo za kinidhamu ni:
i. Sisty Njau – Kaimu Mhandisi wa Wilaya
ii. Damasi Mumwi – Mkuu wa Idara ya Maliasili
iii. Mustafa Magembe – Mkuu wa Idara ya Kilimo na Ushirika
iv. Vinsent Moyo – Mkuu wa Idara ya Ugavi na Ununuzi
v. Mohamedi Songolo – Mkuu wa Idara ya TEHAMA
vi. Sadick Bakari Khatibu – Katibu wa Afya
vii. Tunu Mtamaha – Afisa Ugavi na Ununuzi aliyehamishiwa Halmashauri ya Wilaya Kilwa.
Aidha, Mhe. Waziri ameelekeza kuanzia sasa Maafisa wote wenye kesi za rushwa na ubadhirifu wasihamishwe vituo vyao vya kazi mpaka mashauri yao yanapokamilika.
“Afisa yeyote mwenye kesi ya uhujumu uchumi au ubadhirifu wakati kesi yake ikiendelea ataendelea kuchunguzwa mwenendo wake na hukumu yake ikitoka hatopewa tena jukumu la Ukuu wa Idara au Kitengo hadi mwenendo wake utakaporidhisha” amesema Mhe. Mchengerwa.