Mahakama kuu ya Tanzania kanda ya Morogoro imewatia hatiani wastakiwa watatu na kuwahukumu kwenda jela baada ya kukiri kosa la kuua bila kukusudia katika shauri namba 22 mwaka 2023
Waliohukumiwa ni mshtakiwa namba moja Daniel Wilson (58) kifungo cha miaka 5 Jela mashtakiwa namba mbili na namba tatu Yasini Victori (25) na Viscal Chiduo (32) kifungo cha miaka 8 kila mmoja kwa kumuua bila kukusudia Aruto Bamisi katika kijiji cha Mnozi Kilosa Mkoa wa Morogoro
Akisoma adhabu hiyo Jaji wa Mahakama kuu ya Tanzania kanda ya Morogoro Messe Chaba amesema, adhabu hiyo ni baada ya uchambuzi wa kina wa pande zote mbili upande wa jamhuri uliokuwa na mawakili watano wakiongozwa na wakili msomi Merry Rundu ambao waliwasilisha pia vielelezo ,ramani ya eneo la tukio na ripoti ya daktari.
Imeelezwa usiku wa kuamkia mei 19, 2022 kijiji cha Mnozi Kilosa Morogoro washtakiwa wote wakiwa katika klabu wakinywa pombe walikula njama na kukubaliana kwenda kumshikisha adabu Aruto Bamisi ambae kwa sasa ni marehemu wakimtuhumu kuwa na mahusiano ya kimapenzi na mke wa mshtakiwa namba moja kinyume na kifungu cha 195 na 198 kanuni ya adhabu sura ya 16 marejeo ya mwaka 2022
Kesi hiyo ilitajwa kwa mara ya kwanza julai 21 mwaka 2023,septemba 4 mwaka huu ikatajwa kwa mara ya kwanza kwaajili ya kusikilizwa na washtakiwa wote walisomewa shtaka moja la kuua kwa kukusudia na kukana shtaka hilo,kabla upande wa utetezi ukiongozwa na wakili Catherini Mushi ukaiomba mahakama kuridhia wateja wao kukiri kosa dogo la kuua bila kukusudia na mahakama kuridhia baada ya upande wa jamhuri kutokuwa na kipingamizi.