Watakwimu nchini wametakiwa kuhakikisha wanakuwa na uwezo mzuri wa kuchambua na kutafsiri matokeo ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 na kuyatumia matokeo hayo Katika kupanga, kufuatilia na kutathmini utekelezaji Mipango na programu mbalimbali za maendeleo ili kufikia uchumi wa Viwanda.
Hayo yameelezwa julai 12,2023 Jijini Dodoma na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Jenifa Omolo kwaniaba ya Waziri wa Fedha wakati akifungua mafunzo ya siku mbili kwa Watakwimu wote Tanzania Bara na Zanzibar ulioandaliwa na Chama Cha Watakwimu Tanzania (TASTA).
Omolo amesema kuwa ni muhimu kwa Watakwimu hao kutumia fursa ya mafunzo hayo ili kuweza Miongoni ni utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano wa Mwaka 2021/22- 2025/26 ambao lengo lake, kwa mujibu wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2025 ni kutufikisha kwenye uchumi wa viwanda.
“Matokeo ya Sensa kama mtakavyoona yatatumika katika kufuatilia na kutathmini utekelezaji wa programu za maendeleo za kikanda na Kimataifa ambayo Tanzania imeridhia,”amesema
“Serikali inasisitiza matumizi ya matokeo ya Sensa kwa kutambua kuwa Nchi yetu inaweza kupata thamani ya uwekezaji mkubwa ulioufanya katika utekelezaji wa Sensa ikiwa tu matokeo ya Sensa yatatumika kwa lengo lililokusudiwa, kama nilivyoeleza, katika kupanga, kutekeleza na kutathmini sera, mipango na programu zetu za maendeleo ambazo zitazingatia hali halisi ya idadi ya watu wetu, kuzingatia maeneo wanayoishi na hali ya mazingira ya maeneo hayo,”Amesisitiza.
Hata hivyo ametoa wito kwa wadau wote wakiwemo wananchi kuwa sehemu ya mchakato wa matumizi ya Matokeo hayo katika kupanga mipango mbalimbali ya maendeleo. Tukifanya hivyo, kama nilivyoeleza, tutaweza kupata thamani ya fedha zilizotolewa na Serikali katika kufanikisha zoezi hilo
Pamoja na mambo mengine amesema mafunzo hayo yatafanyi vyema kama yalivyopangwa, kwa kutimiza malengo yake ya kuwapa uelewa, na hatimaye kusambaza matokeo haya kwa wadau mbalimbali
Kwa Upande wake Mtakwimu Mkuu wa Serikali Tanzania Dk.Albina Chuwa amesema kuwa watakwimu wanatakiwa kwenda katika mlengo mmoja ili kuhakikisha takwimu zinaleta maendeleo Kwa jamii.
“Takwimu hizi zinatakiwa kuleta maendeleo katika jamii muhimu sasa Kwa watakwimu wote kuhakikisha takwimu hizi zinakuwa chachu na zinaleta maendeleo kwa Nchi yetu na jamii nzima,”amesema Chuwa.
Naye Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Salum Kassim Ali amesema watakwimu ndio wanaopanga Mipango ya maendeleo ya Nchi hivyo ni wajibu wao Kila mmoja kuhakikisha Matokeo ya Sensa yanatumika ipasavyo.