Wananchi wa kitongoji cha Nunu katika kijiji cha Msakala kata ya Ziwani Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara wameishukuru Wakala wa Barabara Vijijini-TARURA kwa kuwachongea barabara yenye urefu wa kilometa 14 na kilometa moja kuwekwa lami.
Wakiongea na mtandao huu wananchi hao wamesema kabla ya barabara hiyo kuchongwa walikuwa wanatumia baiskeli na pikipiki kama usafiri mkuu wa eneo hilo, kutokana na magari kutoweza kufika, lakini baada ta barabara hiyo kuchongwa kumeanza kufungua fursa mbalimbali kwa kuwa usafiri utakuwa wa uhakika.
Mwenyekiti wa kijiji cha Msakala Bw. Ismaili Hamisi Liyaya amesema TARURA imefanya kazi kubwa kwa kuwa kutengenezwa kwa barabara hizo kutarahisha shughuli za maendeleo kwenye kijiji hicho.
Naye diwani wa kata ya Ziwani katika halmashauri hiyo Abdallah Saidi Makame amesema, kwenye kata yake kuna barabara nyingi zilikuwa na changamoto lakini, wakala hao wa barabara wamechonga barabara ya Majengo-Moma, Mijohoro -Nunu, na kuweka lami barabara ya Msakala-Msangamkuu.