Jeshi la Polisi limewataka wananchi kuacha kusambaza taarifa za uongo na kuzua taharuki kuhusu ajali ya iliyomhusisha Naibu Waziri wa TAMISEMI Dr Festo Dugange.
Katika taarifa ya Kamanda wa Polisi Mkoani Dodoma ACP Martin Otieno imefafanua kuwa ajali hiyo ilitokea tarehe 26/04/2023 katika barabara ya lyumbu maeneo ya St. Peter Clever wilaya na jiji la Dodoma iliyohusisha gari namba T454 DWV aina ya Toyota Land cruiser iliyokuwa ikiendeshwa na Dk Dugange.
ACP Otieno ametoa wito kwa wananchi kutotoa taarifa bila ya kufanyia utafiti taarifa hizo kabla ya kuzisambaza katika mitandao ya kijamii na kubainisha kuwa lipo macho na makini kufuatilia na kutoa ufafanuzi wa taarifa zozote hivyo wananchi wasisite kufika Polisi na kupata ufafanuzi wa taarifa zozote zinazotiliwa shaka.
Katika ajali hiyo Dk Festo Dugange alikuwa peke yake na yeye ndiye aliyekuwa akiendesha gari hilo na ajali hiyo ilitokea wakati akijaribu kumkwepa Bodaboba aliyevuka barabara ghafla bila ya kuchukua tahadhari kitendo ambacho kilipelekea gari hilo kugonga kingo ya barabara na kupinduka.
“Dk Dugange alivunjika kidole gumba cha mkono wa kulia na kupata majeraha katika mkono huo na amelazwa katika Hospitali ya Benjamini Mkapa akiendelea kupatiwa matibabu na Afya yake inaendelea kuimarika” ilieleza taarifa hiyo
Siku za hivi karibuni Kumekuwa na taarifa za uzushi na upotoshaji katika mitandao ya kijamii kwamba katika ajali hiyo kulikuwa na Mwanamke ambaye majina yake hayafahamiki na kwamba alifariki katika ajali hiyo na pia kudai kwamba ajali hiyo ilihusisha gari ambalo ni mali ya Serikali.