Wananchi wa kijiji cha Mbembati kata ya Lubanda wilaya ya Ileje mkoa wa Songwe wameiomba serikali kusaidia ukamilishaji wa zahanati ambayo wameijenga kwa nguvu zao Ili kuondoa adha ya kufuata huduma ya afya umbali wa kilometa 8 katika kituo cha afya Lubanda.
Wananchi hao wametoa ombi hilo Novemba 7, 2023 Kwa mkuu wa wilaya hiyo Mheshimiwa Farida Mgomi wakati wa mkutano wa hadhara wa kusikiliza kero za wananchi kijijini hapo ikiwa ni mwendelezo wa ziara ya kijiji kwa kijiji kusikiliza na kuzitafutia ufumbuzi kupitia wakuu wa idara kutoka ofisi ya mkurugenzi na wakuu wa taasisi za serikali.
Akisoma taarifa ya kijiji hiko mbele ya mkuu wa wilaya Odeni Kandonga amesema wananchi hao walianza ujenzi wa zahanati hiyo mwaka 2014 ambapo wananchi wamechangiza zaidi ya shilingi milioni 15 pamoja na fedha ya mfuko wa jimbo milioni 4 na shilingi milioni 8 kutoka kwa wahisani.
“Wamama wajawazito wanasafiri umbali wa kilomita 8 kufuata huduma ya kujifungulia katika kituo cha afya Lubanda hali ambayo inawafanya wamama hao kujifungulia majumbani kutokana na shida ya miundombinu kutokuwa rafiki kutoka kijijini hapo mpaka kituo Cha afya” amesema Kandonga.
Akijibu ombi la wananchi wa kijiji hicho mkuu wa wilaya hiyo Mheshimiwa Farida Mgomi amewapongeza wananchi hao kutumia nguvu zao kushiriki ujenzi huo kwa kuchangia fedha zaidi ya shilingi milioni 15 ambapo utakuwa ni mwarobaini wa kupata huduma za afya karibu pindi zahanati hiyo itakapoanza kutoa huduma.
“Kutokana na mwitikio wenu serikali itahakikisha inawaunga mkono kumalizia sehemu iliyobaki hivyo basi mhandisi wa ujenzi atakuja wiki lijalo kufanya tathimini ya eneo la zahanati ilipobaki ili jengo hilo liingizwe kwenye bajeti kwa ajili ya kutenga fedha za kukamilisha na huduma zianze kutolewa,” amesema Mhe.Mgomi.
Katika hatua nyingine Mheshimiwa Mgomi akiwa katika kijiji cha Bwenda kata ya Lubanda kusikiliza kero za wananchi amewapongeza wananchi Kwa kuchangia fedha zaidi ya shilingi milioni 50 ambazo zilitumika kujenga zahanati ambayo inatumika kijiji hapo akiwataka waendelee na moyo wa uzalendo wa kupenda maendeleo.
“Katika taarifa yenu iliyosomwa nimesikia zahanati hii mmejenga kwa nguvu zenu ,na uwingi wenu katika mkutano huu ni ishara ya kupenda maendeleo na kupokea vyema maelekezo kwa viongozi wenu, simamieni umoja wenu kwani umoja ni nguvu na utengano ni dhaifu,” amesema Mheshimiwa Mgomi