Home KITAIFA WANAFUNZI 322 WAHITIMU LUHETI MKOANI NJOMBE,MBUNGE KAMONGA AWATAKA WAKAHESHIMU VIAPO VYAO

WANAFUNZI 322 WAHITIMU LUHETI MKOANI NJOMBE,MBUNGE KAMONGA AWATAKA WAKAHESHIMU VIAPO VYAO

 

Na Mwandishi wetu -Njombe

Taasisi ya mafunzo ya afya Lugarawa (LUHETI) iliyopo katika wilaya ya Ludewa mkoani Njombe imeomba serikali kupunguza ushuru kwenye vifaa na kemikali zinazonunuliwa kwa ajili ya matumizi ya maabara ili kupunguza gharama za uendeshaji wa maabara kwenye vyuo.

Wito huo umetolewa na mkuu wa taasisi hiyo Buteye Dotto Buteye wakati wa mahafali ya 23 kwa wahitimu 322 wa kozi za uuguzi na ukunga,sayansi ya maabara tiba,famasia pamoja na uafisa tabibu waliopo katika chuo hicho.

“Taasisi imeanzisha hii maabara ya kisasa ya kutengeneza dawa maalum zinazokwenda kutumika kwenye mwili wa binadamu yenye uwezo wa kutumiwa na wanafunzi takribani 72 mpaka 100,changamoto kubwa ambazo tunakumbana nazo ni ununuzi wa vifaa tiba pamoja kemikali ambazo wanafunzi wetu wanatumia kwa ajili ya kujifunza tunaomba serikali itunge sera ambazo zitakuwa rafiki katika kuagiza vifaa hivi pamoja na kemikali ikiwezekana ushuru wake uweze kuwa chini”amesema Buteye

Ignasy Magoha ni mtaalamu wa maabara hiyo amesema kazi kubwa ya maabara hiyo ni kwa ajili ya wanafunzi kujifunza ambapo amesema wamekuwa wakiitumia kwa ajili ya utengenezaji wa dawa maalum kwa ajili ya matumizi ya binadamu kwa vibali maalum kutoka kwa daktari.

“Tuna uwezo mkubwa sana wa maabara ambayo ina uwezo wa kuingiza takribani watu 72 mpaka watu 100 na kuwapa wanafunzi wetu uwezo mkubwa sana wa kujifunza”amesema Magoha

Kwa upande wake Richard Kilumile ambaye ni mwalimu wa taasisi hiyo akisoma lisala mbele ya mgeni rasmi,amesema licha ya mafanikio makubwa wanayoyapata lakini pia wamekuwa wakikutana na changamoto kadhaa ikiwemo wanafunzi kuacha masomo kutokana na uchumi wa familia zao kuyumba.

Mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga ambaye ndiye mgeni rasmi katika hafla hiyo ameahidi kuzichukua changamoto ambazo ni za kisera na kwenda kuzifanyia kazi huku pia akitoa wito kwa wanafunzi kujituma na kujifunza kwa bidii ili kwenda kuendana na soko la ushindani kazini.

“Tunahitaji jitihada za pamoja ili kuboresha chuo hiki,yale mambo ya kisera tunakwenda serikalini kuyasemea kwasababu wanafunzi wanaosoma hapa ni watoto wetu”amesema Kamonga

Previous article“WATAALAMU WA HALMASHAURI PELEKENI KISARAWE MLICHOJIFUNZA NANENANE”_ DIBIBI
Next articleBODABODA AUAWA , ACHUNWA NGOZI _ MAGAZETINI LEO JUMATANO AGOSTI 09/2023

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here