OR TAMISEMI
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI ayesimamia elimu, Dkt. Charles Msonde amewaagiza Walimu Wakuu wa shule za msingi na wasimiamazi wa elimu kufuatilia ufundishaji na ujifunzaji shuleni na kuhakikisha wanafunzi wa darasa la kwanza wanamudu stadi ya Kusoma, kuandika na kuhesabu.
Ametoa maagizo jana wakati alipokutana na walimu Wakuu, Maafisa elimu na viongozi wanaosimamia elimu katika Mkoa Songwe kwa ajili ya kuhimiza utendaji kazi na utekelezaji wa mikakati ya serikali ya uboreshaji wa utoaji elimu nchini.
Dkt. Msonde amewaagiza Wakuu wa Shule kuwabainisha wanafunzi Wote wa kuanzia darasa la kwanza mpaka darasa la nne wasiomudu Kusoma, Kuandika na Kuhesabu na kuwawekea mkakati wa kuwasaidia ndani ya muda mfupi kabla yahawajaendelea na masomo mengine.
“Tuhakikishe wanafunzi wote wa darasa la kwanza wajue Kusoma, kuandika na kuheshabu, wakishaingia darasa la pili wanafundishwa kuongeza kasi wakati wa kusoma na kuandika lakini wakifika darasa la tatu ndio tunawapa Msingi wa kushika masomo mbalimbali na sio tena kusoma na kuandika” amsema Dkt. Msonde
Aidha, Dkt. Msonde amewataka walimu wakuu na wasimamizi wa ngazi zote kuondokana na hali ya kufanya kazi kwa mazoea na kuanza kivingine katika mwaka huu wa 2023 na kuhakikisha yasiyowezekana yanawezekana.
Ameeleza kuwa dira ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anataka kuona wanafunzi wote wanakuwa ujuzi na umahili kwa kila ngazi wanayopitia ambapo wenye jukumu la kusaidia Utekelezaji wa jambo hilo ni Walimu.
Amewaagiza Viongozi wa elimu ngazi zote kufanya ufuatiliaji wa mara kwa mara ili kubaini changamoto mbalimbali zinazokabili sekta ya elimu ikiwa ni pamoja na kutatua changamoto na kero za walimu kwa kuwafuata katika vituo vyao vya kazi badala ya kukaa maofisini.
Vilevile, Dkt. Msonde amewataka walimu kutekeleza wajibu wao kikamilifu ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanafunzi wanakuwa na malezi ya bora, ujuzi, maarifa, stadi, uzalendo kwa Taifa lao pamoja na maadili ya Kitanzania.