Home KITAIFA WAKUU WA MIKOA WAOMBWA KUHAKIKISHA ELIMU INATOLEWA JUU YA HAKI, ULINZI, USALAMA...

WAKUU WA MIKOA WAOMBWA KUHAKIKISHA ELIMU INATOLEWA JUU YA HAKI, ULINZI, USALAMA NA USTAWI WA WAZEE

Na WMJJWM, Dodoma

Wakuu wa Mikoa wameombwa kuhakikisha elimu ya kina inatolewa kwa wananchi juu ya haki, ulinzi, usalama na ustawi wa wazee

Maelezo hayo yametolewa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima Juni 07, 2023 akizungumza na wajumbe wa Baraza la Wazee kata ya Mkonze, Mkoani Dodoma kuelekea Siku ya Kupinga Ukatili dhidi ya Wazee inayofanyika kila mwaka Juni 15.

Waziri Dkt. Gwajima amebainisha kwamba
kutokana na kuboreshwa kwa huduma za kijamii nchini idadi ya wazee imeongezeka kutoka 2,507,568 hadi kufikia 5,008,339 ambayo ni sawa na asilimia 8.1 ya Watanzania 61,741,120.

Amesema Serikali imeendelea kuadhimisha Siku ya kupinga Ukatili dhidi ya Wazee kila tarehe 15, Juni ambapo Maadhimisho haya ni muhimu kwa ajili ya kuuhabarisha umma juu ya haki, ulinzi, maendeleo na ustawi wa wazee wetu. Aidha, katika kulinda haki ya wazee kuishi, pia Serikali imeendelea kutekeleza Mkakati wa Kitaifa wa Kutokomeza Mauaji kwa Wazee

“Ninachukua fursa hii pia kuwaomba Wakuu wa Mikoa yote nchini kuratibu maadhimisho haya kimikoa kwa kushirikiana na viongozi wa Mabaraza ya Wazee katika mikoa husika, tunapoelekea Siku ya maadhimisho hayo” amesema Waziri Dkt. Gwajima.

Waziri Gwajima ameendelea kusisitiza, jamii yote kuacha kufanya ukatili kwa Wazee na makundi yote kwa ujumla na amewaomba Wanahabari kutumia kalamu zao kuelimisha na kuendelea kukemea masuala ya ukatili nchini kote.

“Serikali itaendelea kuchukua hatua stahiki kuwashughulikia ipasavyo wale wote watakaobainika kufanya vitendo vya ukatili kwa makundi mbalimbali katika jamii hususani kwa wazee”. ameongeza Waziri Dkt. Gwajima.

Maadhimisho ya Kupinga ukatili Dhidi ya Wazee mwaka huu yatafanyika katika ngazi ya Mikoa kote nchini na Kaulimbiu ni “Wazee Wanastahili Heshima na Usikivu Wetu”

Previous articleAJALI YA FUSO NA NOAH YAJERUHI 8 MIKUMI MOROGORO
Next articleRC MAKALLA:TAMASHA LA BULABO MWANZA KUFANYIKA JUNI 13,2023

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here