Wananchi wa Kijiji cha Mkwaja Wilayani Pangani Mkoani Tanga wamemuomba Mkuu wa Wilaya hiyo Zainab Abdallah kuangalia uwekezano wa kuwaongezea Walimu wa lugha ya Kiingereza kwenye Shule zao za Msingi na Sekondari ili kuwafanya Wanafunzi wengi kufahamu lugha hiyo kwa kuwa wanashindwa kufanya biashara na Watalii na jana wameshindwa kumuuzia maandazi Raia wa kigeni kisa lugha na hata walipowakusanya Wanafunzi kuongea nae nao walishindwa.
Akiongea kwa niaba ya Wananchi hao, Juma Majidi amesema lugha ya Kiingereza imekuwa tatizo kwa baadhi ya Wananchi kwenye Kijiji hicho na washindwe kufanya biashara na Watalii wanaotembelea kwenye maeneo yao.
“Mhe.Mkuu wa Wilaya, Mama zetu siku hizi wamefungua migahawa, wanakuja Wazungu hapa tusaidie ile Shule iwe na Walimu wenye idea ya kuzungumza Kiingereza tuwe na elimu na sisi, Jana tumeshindwa kuuza maandazi kwa Mzungu tatizo ni elimu tumekusanya Watoto wameshindwa kuongea nae yule mzungu mpaka sasa yupo Gesti namuogopa”_alisema Majidi
“Mkuu sisi tunaomba tu mtuongezee Walimu wa lugha ya Kiingereza hapa Shule tutatoa sisi hizo hela za ada kama tatizo ni ada ili Watoto wetu wapate elimu ya Kiingereza yani ungekuja kuzunguza kiingereza hapa sidhani kama ungepata Mwananchi wa kukusikiliza”_alieleza
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Pangani Zainab Abdallah ambaye anaendelea na ziara ya kusikiliza na kutatua changamoto za Wanakijiji wa Vijiji mbalimbali wa Pangani aliyoipa jina la “Twende na Mama Samia Kijiji kwa Kijiji’ amewataka Walimu wa somo la Kiingereza kutumia lugha hiyo ili kuwawezesha Wanafunzi kupata maarifa ya Kiingereza na pia ameahidi Serikali itaongeza Walimu wa lugha hiyo.
CC. Millardayo