Home KITAIFA WAJASIRIAMALI WASOMI TUNDUMA WAMSHUKURU RAIS SAMIA UWEZESHAJI KIUCHUMI

WAJASIRIAMALI WASOMI TUNDUMA WAMSHUKURU RAIS SAMIA UWEZESHAJI KIUCHUMI

 

NA JOSEA SINKALA, SONGWE.

Kikundi cha Vijana wasomi wenye taaluma ya mambo ya ardhi cha Jak Real Estate Investiment walionufaika na mikopo ya asilimia 10 kutoka Halmashauri ya Mji Tunduma mkoani Songwe kimeendelea kukua kiuchumi baada ya kubuni mradi wa uendeshaji shughuli za ardhi ikiwemo kutoa hati na kuuza viwanja vya kupimwa.

Mwenyekiti wa kikundi cha Jak Real Estate Investiment John Ambukeghe Mwasopo amesema kikundi chao kilianza kwa kukopeshwa mtaji wa fedha Sh.milioni 20 kutoka Halmashauri ya Tunduma Momba ambapo sasa kimefikia Shilingi Milioni 60.

Ameeleza kuwa kwa sasa wanafanya kazi za kuwekeza kwenye ardhi, Kuelimisha Jamii juu ya namna bora ya uendelezaji wa ardhi, Kupanga na kupima ardhi, Kufanya uthamini wa mali, Kununua na Kuuza viwanja vilivyopimwa, Kusanifu ramani za majengo, Kupima na kuandaa ramani za miundombinu kama umeme, maji, Barabara na reli pamoja na kutoa ushauri wa kitaalamu kwa masuala yahusuyo Ardhi.

“Tunamshukuru Rais wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha fursa ya mikopo ya 10% kutoka kwenye mapato ya ndani ya Halmashauri, sisi vijana imetusaidia sana kwani hadi sasa kipato cha mwanachama mmoja mmoja kimekua”, John Ambukeghe Mwasopo, Mwenyekiti wa kikundi hicho.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Momba, Mhe. Fack Lulandala amewapongeza vijana hao wasomi kwa maamuzi yao ya kuunda kikundi cha kitaaluma na kunufaika na mkopo wa 10% kutoka Halmashauri.

Pia Mhe. Lulandala ametoa wito kwa vijana wengine kwa ujumla kuunda vikundi kutokana na taaluma zao na Halmashauri itakuwa wadhamini ili waweze kupata mikopo kutoka kwenye Taasisi za kifedha.

Mkuu wa Wilaya ya Momba ameziasa Taasisi za umma na watu binafsi kufanya kazi na kikundi cha Jak Real Estate Investiment ili kiweze kukua zaidi kiuchumi na kuwaajiri vijana wengi zaidi.

“Kwa kweli hapa nimefarijika kusikia Taasisi za umma kama TANESCO, TANROADS, TARURA na Halmashauri ya Mji Tunduma kuwaamini vijana hawa na kufanya nao kazi, asanteni sana Taasisi zote ambao mumefanya kazi na kikundi hiki”, Mhe. Fack Lulandala, ameeleza mkuu wa Wilaya ya Momba mkoani Songwe.

Previous articleTANZANIA NA MALAWI ZAKUBALIANA UJENZI WA MRADI WA UMEME MTO SONGWE
Next articleSERIKALI IMESHAURIWA KUTILIA MKAZO KILIMO IKOLOJIA

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here