Home KITAIFA WAFAMASIA WATAKIWA KUZINGATIA SHERIA, KANUNI NA TARATIBU KATIKA UTENDAJI WA MAJUKUMU YAO

WAFAMASIA WATAKIWA KUZINGATIA SHERIA, KANUNI NA TARATIBU KATIKA UTENDAJI WA MAJUKUMU YAO

 

Na. WAF – DODOMA

Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amewataka Wafamasia nchini kuzingatia sheria, kanuni na taratibu katika utendaji wa majukumu yao ikiwa ni pamoja na kuhakikisha dawa zinazotolewa katika vituo vya afya zinazingatia muongozo wa matibabu na orodha ya Taifa ya dawa muhimu.

Waziri Ummy amebainisha hayo leo Jijini Dodoma katika kilele cha maadhimisho ya siku ya wafamasia pamoja na mkutano wa 14 wa mwaka wa Chama cha wanafunzi Wafamasia Tanzania (TAPSA).

Waziri Ummy amesema, kuna baadhi ya wafamasia wanafanya vizuri lakini wapo wachache ambao wanaenda kinyume na maadili, weledi na miiko ya kazi yao.

Pia, ametoa onyo kwa wafamasia kuacha kuwauzia wananchi dawa bila ya kuwepo kwa cheti ambacho kinathibitisha anatakiwa kupewa dawa kutokana na maelekezo ya daktari.

“Mtu anaenda anapewa tu bila utaratibu, nataka tuende mbele, hebu tujilinde, tulinde hii taalamu yetu ya wafamasia, tuzingatie weledi, nidhamu, kwa sababu kubwa mimi naona ni kuenea kwa usugu wa dawa na tunaenda kutengeneza bomu kubwa la usugu wa dawa.” Amesema Waziri Ummy.

Aidha, amewataka kutoa ushauri ni dawa zipi zinatakiwa kuongezwa katika orodha ya dawa katika ngazi ya chini.

“Tumeitengeneza orodha ya dawa kama mnadhani haipo vizuri tupo tayari kupokea maoni na ushauri ili tuweze kufanyia kazi, tulipitia mwaka huu kuna baadhi ya dawa tumezishusha kama za Kisukari na Pressure kama mnadhani kuna dawa zinatakiwa kupatikana katika ngazi ya chini sisi tupo tayari kupokea maoni yenu,” amesema.

Kwa upande wake Rais wa Chama cha Wafamasia Tanzania (PST) Fadhil Hezekia amesema wanaomba katika maeneo yote yenye Wataalamu wabobezi basi katika uchache wake aweze kuwepo Mfamasia.

 

“Eneo la uhifadhi na utoaji wa dawa isiwe kama ni eneo la stoo kama tunaamua kupeleke huduma za kifamasia basi na maeneo haya yaangaliwe ili yaendane na hadhi,”amesema Rais huyo.

Pia amesema mfumo wa huduma za Afya na muundo wake bado hauakisi katika fani yao hivyo wanaomba watambulike kuanzia katika ngazi za Taifa, Mkoa huku akitaka wasiamamizi wa dawa wapewe wakumbukwe kwenye nafasi za ukurugenzi.

Previous articleRAIS SAMIA: PANGA PANGUA HADI SAFU ITULIE…YANGA YASHTUKA DILI LA DJUMA , BANGALA SIMBA_ MAGAZETINI LEO JUMAMOSI JUNI 17/2023
Next articleSERIKALI YATOA ZAIDI YA SH. BILIONI MOJA KUENDELEZA MIRADI YA UBUNIFU NCHINI

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here