Kwa wakazi wa Jijini Dar es Salaam inaweza kuwa faraja kwa watumiaji wa mabasi yanayomilikiwa na Wakala wa Mabasi yaendayo Haraka (Dart), baada ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kuanza majadiliano na wakala huo kufunga huduma ya intaneti ya bure kwenye vituo vya mabasi hayo.
Huduma hiyo ya intaneti itawahusu wamiliki wa simu janja na vifaa vingine vyenye kuwezesha mfumo wa huo, ambapo abiria atapata fursa ya kuvinjari mtandaoni bure akisubiri basi kwenda kituo kingine.
Kauli hiyo imetolewa leo Novemba 21, 2023 na Ofisa Mtendaji Mkuu wa UCSAF, Justina Mashiba katika kikao kazi na wahariri na waandishi wa habari jijini hapa.
“Tupo kwenye mazungumzo na Dart kwa ajili ya kuunganisha inatneti ya bure kwenye vituo vya mabasi yaendayo haraka, lakini huduma hii baadaye itakuwa ya kuchangia kidogo,”amesema.
Baadhi ya maeneo ambayo tayari wanafurahia huduma hiyo ya intaneti ya bure iliyofungwa na mfuko huo ni Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es Salaam na mpango uliopo ni kufunga huduma hiyo soko jipya la Mwenge Dar es Salaam.
Akizungumzia huduma za mawasiliano vijijini, Mashiba amesema UCSAF imeingia mikataba na kampuni za simu kufikisha huduma ya mawasiliano katika kata 1974 zenye vijiji 5,111.
Justina amesema katika vijiji hivyo kutajengwa minara 2,149 na itakapokamilika wananchi takribani 23,798,848 watapata huduma ya mawasiliano ya simu kwa uhakika.
“Mpaka sasa, jumla ya kata 1,197 zenye wakazi 14,572,644 wameshafikishiwa huduma ya mawasiliano kupitia minara 1,321 iliyojengwa katika kata hizo,”ameeleza.
Kwa eneo la tiba mtandao, Justina amesema, UCSAF inatekeleza mradi huu kwa kushirikiana na Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI).
“Hospitali nyingine zilizounganishwa ni pamoja na Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Morogoro RRH, na zinazokamilishwa ni Hospitali ya Rufani ya mkoa wa Ruvuma, Tanga, Katavi, Nzega na Chato,
“Kwa upande wa Zanzibar tunaunganisha Hospitali ya Abdala Mzee iliyopo Pemba na Hospitali ya Rufaa ya Mnazimmoja iliyopo Unguja ambapo utekelezaji wake upo katika hatua za mwisho,”amesema.
Kuhusu teknolojia za simu, Justina amesema asilimia 92 ya wananchi vijijini na mijini, wamefikiwa na huduma ya 2G kwa asilimia 96, 3G asilimia 77 na 4G kwa asilimia 65.
Akizungumzia hatua hiyo, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF), Deodatus Balile ameiomba UCSAF ihakikishe huduma ya mtandao wa 3G na 4G zinawafikia wananchi wengi zaidi