Home KITAIFA VIONGOZI WA DINI WATAKIWA KUKEMEA UKATILI WA KIJINSIA

VIONGOZI WA DINI WATAKIWA KUKEMEA UKATILI WA KIJINSIA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka viongozi wa dini kila wanapopata nafasi kwenye mimbari wakemee kuhusu ukatili wa kijinsia pamoja na wale wanaoenda kinyume na maadili na desturi za Kitanzania.

“Nitoe rai kwa viongozi wetu wa dini muendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa kulinda mila, desturi na tamaduni za Kitanzania hususan katika kipindi hiki tunachokabiliwa na wimbi kubwa la mmomonyoko wa maadili,” amesema.

Ametoa wito huo leo (Jumapili, Aprili 2, 2023) wakati akizungumza na viongozi na waumini waliohudhuria mashindano ya kitaifa ya kuhifadhi Quran tukufu yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, jijini Dar es Salaam. Mashindano hayo yaliandaliwa na taasisi ya Aisha Sururu Foundation (ASF).

“Sasa hivi Tanzania inakabiliwa na tatizo la mmomonyoko wa maadili na pia kumeibuka wimbi la vitendo vingine ambavyo vinakwenda kinyume kabisa na dini zetu pamoja na mila, desturi na tamaduni za kitanzania. Ninampongeza sana Dkt. Aboubakar bin Zubeir, Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania kwa kulisimamia kidete suala hili ikiwa ni pamoja na kutoa maelekezo mahsusi kwa viongozi wote wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania kulikemea na kutolifumbia macho.”

“Tunapowahifadhisha Quran vijana wetu, tuhakikishe jambo hilo jema linakwenda sambamba na ujenzi wa misingi imara ya malezi itakayowafanya wawe raia wema, waadilifu na wazalendo kwa nchi yao. Tukiwa wazazi, walezi na walimu wa Quran, nitoe rai kwamba tunapotoka hapa hebu tujiulize ni kwa kiasi gani tunaizingatia hii Quran tukufu katika mwenendo mzima wa maisha yetu ya kila siku.”

Waziri Mkuu amesema kwa kufanya hivyo watakuwa wanamsaidia Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye mara zote amekuwa akiguswa na suala zima la maadili hususan kwa vijana. “Pia tutamsaidia Mheshimiwa Rais kupata wasaidizi wacha Mungu na waadilifu katika kutekeleza majukumu yao ya kuwahudumia wananchi.”

“Nasi tuendelee kuiombea nchi yetu na viongozi wake ili waendelee kuliongoza vema Taifa letu ikiwa ni pamoja na kujenga umoja na mshikamano, kudumisha amani na kuimarisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii,” amesisitiza.

Previous articleNaCONGO LATOA TAMKO JUU YA TUHUMA YA BAADHI YA MASHIRIKA KUTUHUMIWA KUENEZA MASWALA YA USHOGA
Next articleVIGOGO WAWEKWA MATUMBO JOTO: SOMA HAPA HABARI ZILIZOPO KWENYE MAGAZETI YA LEO JUMATATU APRILI O3/2023

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here