Na Mwandishi wetu -Njombe
Vijana wametakiwa kuandaa vizuri maisha yao kwa kujenga uchumi ikiwemo kulima matunda ya Parachichi ili kutengeneza kizazi imara kutokana na uchumi imara watakaoweza kuutengeneza wakati wa ujana na kuondoa utegemezi wakati nguvu zao zinapopungua.
Wito huo umetolewa na Diwani wa kata ya Utalingolo ambaye pia ni mwenyekiti wa halmashauri ya mji wa Njombe wakati wa uzinduzi wa michuano ya Mpete diwani Cup kata ya Utalingolo iliyozinduliwa katika kata hiyo.
“Michezo inatafsiri kubwa sana kwa vijana,vijana ni taifa la sasa inatakiwa tuandae maisha kwa ajili ya baadaye na tujue kwamba baadaye sisi ndio tutakuwa wazazi kwa hiyo lazima tuandae maisha yetu kwa kukuza uchumi tukiwa na afya”amesema Erasto Mpete
Aidha katika michuano hiyo kampuni ya Mtewele General Traders imeongeza kitita cha shilingi laki tano (500,000) kwenye michuano ya Mpete Diwani Cup ili kuimarisha na kuongeza ushindani wa michuano hiyo.
Deo Mtewele kwa niaba ya mkurugenzi wa kampuni amesema kampuni hiyo imewiwa kutoa kiasi hicho ili kuunga mkono juhudi za diwani wa kata ya Utalingolo Erasto Mpete kutokana na jitihada zake za kuendelea kuimarisha uchumi pamoja na michezo kwa wananchi wa Utalingolo.
“Upendo unaanzia nyumbani na mtu hawezi kuwa mdau wa maendeleo nyumbani kama hapewi nafasi ya kushirikishwa kwenye hilo tunakupongeza sana diwani na kwa kusema hicyo sisi tumewiwa kuchangia shilingi laki tano kwa ajili ya ghalama za fainali”amesema Deo Mtewele.
Afisa michezo wa halmashauri ya mji wa Njombe Clemence Manga ameto pongezi kwa kazi kubwa inayofanywa na diwani wa kata hiyo kwa vijana kwa kuwa amekuwa mstari wa mbele kukuza michezo huku akishukuru pia wananchi wa kata ya Utalingolo kufanya vizuri kwenye mapokezi ya mwenge ndani ya kata hiyo.
Michuano ya Mpete Diwani Cup imezinduliwa katika uwanja wa Ruhuji uliopo kwenye kata hiyo kwa mtanange uliokutanisha timu ya Utalongolo FC dhidi ya Mfereke FC.