Home KITAIFA VIJANA SIHA WASHAURIWA KUCHANGAMKIA FURSA ZA MIKOPO ISIYOKUWA NA RIBA

VIJANA SIHA WASHAURIWA KUCHANGAMKIA FURSA ZA MIKOPO ISIYOKUWA NA RIBA

Vijana wilayani Siha Mkoani Kilimanjaro wameshauriwa kujiunga kwenye vikundi na kujitokeza kwa wingi katika kuchangamkia fursa za mikopo ya 4% isiyokuwa na riba inayotolewa na Halmashauri na kuweza kubuni fursa zitakazo wakwamua kiuchumi na kukukuza uchumi wao badala yake kuacha kubweteka na kujiingiza katika makundi maovu ya utumiaji madawa ya kulevya hali ambayo inachangia kuharibu vijana ambao ndio nguvu kazi ya Taifa.

Hamasa hiyo imetolewa katika tamasha la maadhimisho ya Siku ya vijana Duniani
ambapo kwa Wilaya hiyo maadhimisho hayo yalifanyika Kata ya Sanya Juu katika ambapo Mkurugenzi mtendaji wa shirika la kijamii lisilo la kiserikali linalojishughulisha na kuchochea ukuaji wa uchumi wa jamii na kuimarisha ustawi wa jumla kwa vijana , wanawake ,familia na jamii (Empact foundation) Tumsifu Kweka alisema tamasha hilo limeandaliwa na shirika hilo kwa kushirikiana na Halmashauri ,kwa lengo la kuwakusanya vijana ili waweze kupata elimu juu ya mambo mbalimbali kwani vijana ndio tegemeo la Taifa lakini ndio eneo ambalo lina changamoto nyingi lakini kupitia warsha hiyo tunaamini inaweza kwa kiasi kuwa saidia vijana kujitambua na kuona namna gani ya kufanya mambo katika shughuli zao za kila siku kwenye maeneo yao .

“Ninawashauri vijana kujitambua na kuwa na maadili kwenye Taifa letu kwani vijana ni kundi muhimu ambalo lazima tulitazame kwasababu vijana wa leo ndio wanaenda kuwa wazee wa kesho kwahiyo tukiandaa vijana wazuri leo tunatengeneza Taifa lililo bora hivyo hatuna budi kuona umuhimu wa kwenda kwenye shughuli zilizo rasmi na kuondoka huko ambako sio kuzuri kama ilivyo kwenye madawa na ninawaomba viongozi wa dini kuendelea kuwahimiza vijana kuwa na maadili mema na kuendelea kujitambua na kuchangamkia fursa za mikopo na kubuni fursa za maendeleo zitakazo wakuza vijana kiuchumi ili Taifa liweze kuwa na vijana bora kwaajili ya Taifa letu” alisema Kweka

Mkuu wa Wilaya hiyo Christopher Timbuka alisema kuwa Serikali inaendelea kuwasisitiza vijana kujikita katika shughuli za uzalishaji ambazo zitawaongezea kipato na kuwaletea maendeleo badala ya kujihusisha shughuli ambazo zinawapelekea kuwa na mda mwingi wa kukaa bila kufanya kazi na hivyo kuishia kuingia katika matamanio ya kutumia madawa ya kulevya.

“Tayari serikali imeanza jitihada za kuwaelimisha vijana kupitia idara ya maendeleo ya jamii kuwaelimisha vijana waweze kujiunga kwenye vikundi waweze kupata mikopo ambayo inafaida mbili ikiwa ni pamoja na mashariti yake ni nafuu,mikopo haina riba ukilinganisha na taasisi nyingine za fedha ambazo masharti yao yana mlolongo mrefu na pia kuna riba,hivyo tunatumaini baada ya muda mfupi vijana wengi watajitokeza kujiunga katika vikundi ili waweze kupata mikopo hiyo kama ambavyo tumewaasa”alisisitiza.

Kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri hiyo Haji Mnasi amesema fursa za mikopo zipo ila makundi ya vijana kuchangamkia fursa za mikopo muitikio umekuwa mdogo, lakini makundi ya wanawake wamekuwa mstari wa mbele katika kuchangamkia fursa hivyo yeye kwa kushirikiana na wataalamu wake watahakikisha kwamba elimu inazidi kutolewa kwa vijana ili waweze kujitokeza kwa wingi na kuchukua mikopo hiyo isiyokuwa na riba lakini pia waweze kuirejesha kwa mujibu wa sheria na taratibu ambazo zipo, ambapo amesema wamekuwa wakiendele kupambana kuwajengea uwezo vijana kuwa wabunifu kuwa vichocheo kuweza kujishughulisha kuzalisha mali ili kuondokana na suala zima la mihadarati , kujiingiza katika madawa ya kulevya licha ya kuwa tumekuwa tukiendelea kutoa elimu na hamasa ya kutosha kwa vijana kushiriki kuchukua mikopo.

Miongoni mwa vijana walioshiriki katika maadhimisho ya siku ya vijana duniani Emanuel Msusa amewashauri vijana wenzake kuwa uthubutu katika mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na uthubutu wa shughuli za biashara,ujasiriamali pamoja na mambo ya kijamii lakini pia wawe na imani kuwa wanaweza huku Hilda Gasper ambaye ni mmoja wa vijana aliyeshiriki katika siku hiyo akiwashukuru waandaaji tamasha hilo kuwakutanisha katika siku ya vijana duniani na kusema kuwa siku hiyo imekuwa siku ya kujifunza mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na ukumbushwa mchango na wajibu katika maendeleo ya jamii na Taifa.

Previous articleKAMERA KUFUNGWA KITONGA NA MAJINJA KUKABILIANA NA AJALI IRINGA
Next articleNAIBU WAZIRI UMMY, ATOA WITO KWA WANANCHI KUTEMBELEA VIVUTIO VYA UTALII

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here