Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi (UWT) Zainabu Shomari amewataka Watanzania kupuuza baadhi ya hoja zenye malengo ya kupotosha umma zinazotolewa na watu mbalimbali juu ya maridhiano ya uendelezaji wa bandari baina ya Tanzania na DP World.
Amebainisha hayo mkoani Njombe wakati akizungumza na wananchi wa mtaa wa Kambarage mjini Njombe mara baada ya kukagua miradi mbalimbali inayotekelezwa na Serikali pamoja na UWT wilaya ya Njombe.
“Ndugu zangu nawaombeni tusisikilize maneno ya propaganda ya kutaka kumchafua Rais wetu kwa ubinafsi wao kwasababu siku nyingi walikuwa hawana la kusema”amesema Zainabu Shomari
Vilevile amewapongeza wabunge kwa kuridhia makubaliano hayo kwa kuwa nchi inahitaji maendeleo
“Tunawapongeza sana wabunge kwa kuridhia makubaliano ya ushirikiano baina ya TPA na DP World,ninyi ndio wawakilishi wa wananchi na mliona kwamba kuna haja ya kufanya vile kwasababu nchi inataka maendeleo”alisema Zainabu Shomari
Aidha amekosoa baadhi ya Watanzania na wanasiasa wanaopotosha umma kwa kutoa maneno ambayo sio ya kiungwana na yenye nia ya kumchonganisha Rais Samia na Wananchi.
“Maendeleo hatuwezi kuyapata bila ya kuwa na mapato mazuri,mwanamke yule (Rais Samia) anahangaika kuitafutia nchi yake mambo mazuri wanatokea wanaume wanasema Rais anataka kuuza nchi”Amesema Zainabu Shomari Makamu Mwenyekiti wa UWT Taifa
Katika hatua nyingine Makamu Mwenyekiti amekemea dhidi ya kauli zenye lengo la kubaguana;
“Samia Suluhu ni Mtanzania hakuna ubaguzi, mtoto wa kiume anasimama anasema kesho kutwa watakuja waarabu watatutawala maana yake kauza nchi kwanini haendi kuuza kwao lakini uwatizame na wanaume wenyewe wameshakaa nchi nyingi za Ulaya ambao wanaunga mkono mambo ya kuoana jinsia moja”