Jumuiya ya umoja wa wanawake wa Chama cha Mapinduzi (UWT) mkoa wa Njombe imesema kutokana na umoja wa timu ya Chama cha Mapinduzi kwa sasa wanaamini kwenda kupambana na kuchukua kata tatu kati ya 26 ambazo zinaongozwa ngazi ya udiwani na vyama vya Upinzani.
Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Scolastika Kevela amebainisha hayo wakati akizungumza na viongozi wa jimbo la Ludewa alipofika wilayani humo kwa ajili ya ziara yake ya kawaida ya kuimarisha Chama na Jumuiya ambapo amezitaja kata hizo kuwa Ruhuhu inayoongozwa na ACT,Lupingu CHADEMA pamoja Lumbila iliyopo pia CHADEMA.
“Hapa kuna kata tatu zipo upinzani lakini kwa timu na umoja tulionao nina imani tunaenda kufuta upinzani kwenye hizi kata na kuzirudisha kwenye himaya ya Chama cha Mapinduzi,na watu watatufuata kwa matendo na kazi zetu nzuri ila kama tukionekana ni wala rushwa tutakuja kupingwa”amesema Scolastika Kevela.
Sambamba na hilo mwenyekiti ametoa wito kwa wananchi mkoani Njombe kupunguza ukarimu uliopitiliza ili kuzuia matukio ya ukatili ambayo yamekuwa yakijitokeza kwenye jamii.
“Tufute ule utamaduni wa ukarimu uliopitiliza,watu wengine wanakuja kwenye familia zetu lakini ni matapeli,kuna watu unawakarimu unampa chumba mgeni wakati wa usiku kwa ajili ya kupumzika na kwa bahati mbaya ndio chumba hicho hicho cha watoto halafu wanaharibu watoto wetu”aliongeza Scolastika