Njombe
Jumuiya ya umoja wa vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Njombe imejitokeza na kulaani vitendo na kauli zinazoonekana kuwa za ubaguzi zilizotolewa na baadhi ya viongozi wa siasa ambazo zinaweza kuwagawa Watanzania.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Njombe, Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Samuel Mgaya amesema Umoja wa vijana haukubaliani na kauli hizo huku akitolea mfano wa kiongozi mmoja wa chama cha upinzani ambae hakumtaja waziwazi, ambapo amesema kitendo hicho kinaweza kuligawa taifa ambalo lina misingi ya Udugu,Umoja na mshikamano ambao uliasisiwa na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere
“Kiongozi mkubwa wa Chama cha siasa amesikika wazi akitoa kauli za ubaguzi dhidi ya Watanzania wanaotokea Zanzibar tena akiwalenga watu kwa majina na nafasi zao wanazozitumikia na tunajua wapo wafuasi wengine wachache wameandika maneno yanye vimelea vya kubagua Watanzania”Amesema Mgaya
Mgaya ameongeza kuwa “Kauli iliyotolewa na kiongozi huyu ikifuatiwa na wafuasi wake wachache inastahili kukemewa,kulaaniwa na kupingwa kwa nguvu zote kadri inavyowezekana ili kulinda utulivu tulio nao”
Amesema serikali ina dhamira njema ya kufanya uwekezaji wenye tija katika bandari zetu kutokana na kukua kwa teknolojia na hivyo Watanzania hawapaswi kubeza jitihada hizo za Rais Daktari Samia Suluhu Hassan.
Wanasiasa mbalimbali wameendelea kujitokeza kupitia vyombo vya habari kupinga kauli zinazodaiwa kuwa ni za ubaguzi zilizotolewa na mwanasiasa huyo nguli wa upinzani kutokana na sakata la makubaliano ya kwenda kuendeleza bandari kupitia Kampuni ya DP World ya nchini Dubai.