Home KITAIFA UTEKELEZAJI WA SUALA LA NISHATI SAFI NA SALAMA NI WAJIBU REA –MHANDISI...

UTEKELEZAJI WA SUALA LA NISHATI SAFI NA SALAMA NI WAJIBU REA –MHANDISI SAIDY

 

Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Saidy amesema REA kama taasisi ya serikali na mmoja wa wadau katika masuala ya nishati safi na salama ina wajibu wa kuhakikisha inawezesha upatikanaji wa nishati safi na salama ya kupikia vijijini kwa sababu Sheria ya uanzishaji wa REA imeweka msingi wa kuendeleza nishati safi ya kupikia kwa Watanzania wa vijijini.

Mhandisi Hassan Saidy ameyasema hayo kwenye semina kuhusu matumizi ya nishati safi na salama kwa wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; semina iliyofanyika kwenye ukumbi wa Pius Msekwa katika viwanja vya Bunge jijini Dodoma, tarehe 27 Mei, 2023.

Mhandisi Saidy amesema hayo wakati akitoa mada kuhusu matumizi ya nishati safi na salama ya kupikia na kuongeza kuwa nishati ya kupikia utumiwa na Watanzania wengi na kwamba msingi wa kuhamasisha, kuendeleza na kuwezesha matumizi ya nishati safi ya kupikia lipo kwenye Ilani ya Chama Tawala (Chama cha Mapinduzi – CCM) ya Mwaka 2020, lipo kwenye Sera ya Taifa ya Nishati, Sera ya Taifa ya Utunzaji na Uhifadhi wa Mazingira pamoja na Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa ambapo miongozo yote hiyo, inahamasisha matumizi ya vifaa bora, kwenye kutumia nishati safi, salama na endelevu kwa Watu wote lakini pia inasisitiza katika kuachana na matumizi ya mkaa usio salama na nishati zote chafu.

“Na sisi (Wakala wa Nishati Vijijini – REA); Sheria ya REA inatupa wajibu wa kuhakikisha tunawezesha upatikanaji wa nishati safi na salama kwa Watu vijijini na si umeme tu, ni nishati zote”.
Alisema Mhandisi Saidy.

Mhandisi Saidy amesema utekelezaji wa suala la nishati safi na salama ya kupikia, utaliwezesha Taifa kufikia Malengo la Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa ya Mwaka 2030 hususan lengo namba 7; ambalo linahusu upatikanaji wa nishati safi na ya uhakika, nafuu na endelevu.

Mhandisi Saidy, ameongeza kuwa hali ya matumizi ya mkaa na kuni kwa Watu wa vijijini ipo juu na kuongeza kuwa kati ya asilimia 91 hadi 99 Wananchi wa vijijni, wanatumia nishati isiyo safi na salama.

Mkurugenzi Mkuu, Hassan Saidy amesema Serikali itaendelea kuwaelimisha Wananchi kwanza kutambua nishati safi na salama na nishati chafu na athari zake kiafya, kimazingira, kiuchumi kwa wale wanaotumia nishati chafu na kwamba Wakala wa Nishati Vijijini (REA) itaendelea kuwezesha upatikanaji wa nishati safi na salama kwa Watanzania wa vijijini na si umeme tu.

Semina kwa wabunge ni sehemu ya jukwaa la kutoa elimu na hamasa kwenda kwa Wananchi na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) itaendelea kufanya hivyo kwa kadri fursa ya kufanya hivyo, itakapopatikana

Previous articleTEMBO NICKEL KUANZA UZALISHAJI MWAKA 2026
Next article“HATUJAMALIZA TUKUTANE ALJERIA” _MAGAZETINI LEO JUMATATU MEI 29/ 2023

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here