NA JOSEA SINKALA, SONGWE.
Maadhimisho ya siku ya Kimondo Duniani yaliyokuwa yafanyike Juni 29, 2023 Mkoani Songwe yameingia dosari baada ya Mamlaka ya hifadhi Ngorongoro (NCAA) kuhamishia mkoani Mbeya.
Maadhimisho ya siku ya kimondo yalianza kuadhimishwa mwaka 2017 Mkoani hapa, ambapo huambatana na maonesho ya biashara ya siku tatu na kuhitimishwa na kongamano la kisayansi kuhusu elimu ya utalii wa anga na uhifadhi wa mali kale.
Hata hivyo, katika hali ya kushangaza kongamano hilo la kisayansi kuhusu elimu ya utalii wa anga na uhifadhi wa mali kale lililopangwa kufanyika Juni 29, 2023 katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Songwe ghafla lilihamishiwa Mkoani Mbeya.
Taarifa kutoka ndani ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Songwe zinaeleza kuwa hali ya kuhamishwa kwa kongamano hilo kwenda kufanyikia Mkoa jirani wa Mbeya kumetokana na kile kilichoelezwa kuwa huenda Mamlaka hiyo inakwepa agizo la Serikali ya Mkoa iliyoagiza kulipa fidia kwa wananchi wanaotakiwa kupisha utanuzi wa eneo hilo kabla ya maadhimisho hayo.
Mmoja wa viongozi wa Mamlaka hiyo ya Ngorongoro, Joshua Mwankunda anayehusika na shughuli za urithi wa utamaduni na mali kale licha ya kukiri kongamano hilo kuhamishiwa Mkoani Mbeya, amesema hakuna ombwe lolote lililojitokeza kati ya Mamlaka hiyo na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
Hata hivyo, Mwankunda alipotakiwa kueleza sababu za mamlaka hiyo kuhamishia kongamano hilo Mkoa wa Mbeya, amesema kwa ufupi kuwa kumetokana na Mkoa wa Songwe kutokuwa na miundombinu mizuri ya kuwezesha wadau wa kongamano hilo waliopo nje kulifuatilia.
“Hakuna ombwe lolote la mawasiliano kati yetu na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na wala kuhamishwa kwa kongamano hili hakusiani kabisa na mambo ya ulipaji wa fidia, hivyo naomba uwasiliane na Ofisa habari ambaye ndiye msemaji wa taasisi kwani mimi ni mfanyakazi ninayehusika kuratibu tuu shughuli hizo”, Joshua Mwankunda.
Kwa upande wake, Ofisa Habari wa Mamlaka ya Ngorongoro, Joyce Mgaya alipotafutwa kutolea ufafanuzi wa kina kuhusu kutokea kwa ombwe la kimawasiliano kati yao na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Songwe, amesema hakuna tatizo lolote na kwamba Ngorongoro waliamua kuhamishia kongamano hilo Mkoa wa Mbeya kwa sababu wadau wengi wa kongamano hilo wanapatikana mkoa huo wa Mbeya.
“Nakuhakikishia hakuna tatizo lolote na maadhimisho yatafanyika hapo Songwe na mimi niko njiani nakuja hapo Songwe na kila kitu kinaenda kama kilivyopangwa” alisema Mgaya.
Akizungumzia suala la wananchi kulipwa fidia, Mgaya amesema fedha kwa ajili ya malipo zipo tayari na wakati wowote wananchi hao wataanza kulipwa fedha zao.
Wakati Ngorongoro wakijibu hayo, taarifa za uhakika kutoka ndani ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Songwe zinaeleza kuwa ombwe la mawasiliano limetokana na mambo makuu mawili ambayo ni mamlaka hiyo kushindwa kuushirikisha mkoa katika maandalizi kuanzia hatua za awali, pamoja na Mamlaka hiyo kushindwa kutekeleza makubaliano ya waliyokubaliana ya kutaka wananchi wanaotakiwa kupisha utanuzi wa hifadhi walipwe kwanza fidia ndipo sherehe hizi za maadhimisho zifanyike.
“Wananchi hawa wamekuwa wavumilivu kwa muda mrefu sana na tulikubaliana kabla ya maadhimisho kufanyika ni lazima wananchi walipwe fidia zao, sasa leo unaenda kufanya sherehe kwenye eneo ambalo wananchi wanakilio cha kutolipwa fedha zao kwa wakati, huku makazi yao yakiwa yamebolewa” kilisema chanzo hicho.
Machi 2023 Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) Jenerali Mstaafu Venance Mabeyo, aliwataka wananchi wa Kitongoji cha Isela Kijiji cha Ndolezi Wilayani Mbozi kuendelea kuwa na subira kwani Serikali imedhamiria kuwalipa wananchi wote waliokubali kuachia ardhi zao kwa ajili ya kupisha upanuzi wa kituo cha utalii cha Kimondo.
Amesema tayari Serikali kupitia Mamlaka hiyo ya Ngorongoro imetenga kiasi cha shilingi bilioni 1.4 kwa ajili ya kulipa fidia wananchi zaidi ya 179 waliokubali kwa hiyari yao kupisha upanuzi wa kituo hicho cha Kimondo.
Jenerali Mabeyo amelazimika kutoa kauli hiyo baada ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Songwe Radwell Mwampashi, wakati akitoa salamu za chama kwenye tukio hilo kuomba Mamlaka ya Hifadhi Ngorongoro kuharakisha zoezi la ulipaji fidia kwa wananchi waliopisha upanuzi wa eneo hilo la kimondo.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Songwe Dkt . Francis Michael, amesema katika kilele cha kuazimisha Siku ya Kimondo Duniani mwaka 2019 Serikali iliagiza kuboresha eneo la Kimondo cha Ndolezi Mbozi kwa kuanzisha kituo cha taarifa za utalii yaani makumbusho ambayo yamezinduliwa.