Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amewasimamisha kazi watumishi wa afya wa hospitali ya Kaliua Mkoani Tabora ili kupisha uchunguzi kufuatia tukio la watoto mapacha kudaiwa kuuwawa na kunyofolewa Macho.
Hatua hii inafuatia taarifa iliyosambaa mtandaoni kutoka kwa Baba wa watoto hao Kisaka Mtoisenga aliyeeleza kuhusu vifo tata vya watoto hao pamoja na matukio ya kuchukuliwa viungo vyao.
“‪Tulipotoka nje (kwaajili ya maziko), kabla ya kupanda gari tulifungua maboksi yaliyokuwa na miili ya watoto tukakuta watoto wameng’olewa macho, wamekatwa ulimi na wamechunwa ngozi kwenye paji la uso.Tukahamaki na kurudi hospitalini kuuliza lakini hatukupata majibu ya kuridhisha‬”
Waziri wa Afya kupitia ukurasa wake wa Twitter amesema uchunguzi uliofanyika umebaini kuwa jambo hilo ni la kweli na kumuagiza Mganga mkuu wa Mkoa wa Tabora kusimamia vyema weledi, maadili na miiko ya watumishi wa afya walio chini yake