

Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa uwanja wa ndege wa Msalato jijini Dodoma unaendelea kwa kasi ambapo hadi sasa utekelezaji wake umefikia asilimia 18.5 huku ukitarajiwa kukamilika mwezi Aprili, mwaka 2025.
Hayo yamesemwa Aprili 17, 2023 na Mhandisi wa miradi kutoka Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Dodoma, Mhandisi Colman Gaston akiongea na waandishi wa habari ambao amesema, utekelezaji wa mradi huo utahusisha sehemu mbili za ujenzi
Mhandisi Colman amesema,sehemu ya kwanza ya ujenzi unahusisha ujenzi wa miundombinu mbalimbali ikiwemo sehemu ya kurukia ndege (run way), sehemu za kupaki ndege.
“Mradi wa ujenzi wa uwanja wa ndege wa Msalato unahusisha ujenzi wa sehemu ya kurukia ndege (run way), sehemu za kupaki ndege (tax way) na maegesho (apron” alisema Mhandisi Colman na kuongeza kuwa
“Pia mradi huo utahusisha ujenzi wa fensi na miundombinu ya umeme pamoja na miundombinu ya kuzima moto.”

Kuhusu sehemu ya pili ya utekelezaji wa mradi huo, Mhandisi Colman amesema,
“Katika sehemu ya pili utahusisha ujenzi wa jengo la abiria (terminal building), mnara wa kuongozea ndege (observation tower) ambapo katika sehemu hii utekelezaji wake mkandarasi ni China Beijing na mradi utagharimu kiasi cha shilingi Bilioni 194”

Kukamilika kwa uwanja wa ndege wa kimataifa Msalato jijiji Dodoma, kunatajwa kuwa chachu ya kubadili mandhari ya jiji hilo, kwani ndege zote ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Ulaya zitatua moja kwa moja katika uwanja huo badala ya Dar es Salaam kama ilivyozoeleka.