Home KITAIFA UJENZI WA BOMBA LA GESI KUTOKA BANDARINI HADI KIWANDA CHA ORYX KIGAMBONI...

UJENZI WA BOMBA LA GESI KUTOKA BANDARINI HADI KIWANDA CHA ORYX KIGAMBONI WAKAMILIKA

 

Na Mwandishi Wetu

KAMPUNI ya Oryx Gas Tanzania imekamilisha ujenzi wa bomba kubwa la kusafirisha nishati ya gesi kutoka kwenye meli bandarini kwenda kwenye kiwanda cha gesi ya kampuni hiyo kilichopo eneo la kigamboni jijini Dar es Salaam na hivyo kupunguza muda wa kupokea gesi bandarini.

Kukamilika kwa ujenzi wa bomba hilo kubwa lenye ukubwa wan chi 10 linakwenda kusaidia pia kurahisha utoaji huduma kwa wateja wakubwa wa gesi wa gasi ya Oryx ambao walikuwa wanalazimika kutumia muda mwingi kusubiri gesi itolewe kwenye meli.

Akizungumza jana Juni 23,mwaka 2023 mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Meneja Miradi wa Oryx Gas Tanzania Joseph Soka amesema Juni 17 mwaka huu ndio wamekamilisha ujenzi wa bomba la kupokelea gesi kutoka KOJ kwenda depo ya Oryx Gas iliyopo Kigamboni.

“Hapo tulikuwa na bomba dogo lenye ukubwa wa nchi sita na sasa tuna bomba lenye ukubwa wa nchi 10.Faida za mradi huu ni katika kuanza mpango wa kwanza wa kuongeza ufanisi na operesheni ya uuzaji wa gesi kwa ujumla.

“Kwa maana tulipokuwa tunatumia bomba dogo tulikuwa tunapokea mzigo kutoka katika meli kwa muda usiopungua saa 30 kwa mzigo wa metriki tani 2,500.Baada ya kuongeza ukubwa wa bomba la kupokelea gesi sasa tunaweza kupokea ujazo ule ule wa kwa muda uliopungua hadi saa 20.

“Kwa hiyo tumeweza kupunguza muda wa meli kusubiria bandarini katika kushusha ili kurudi na kwenda kuchukua mzigo mwingine, lakini zaidi tuna mabomba mawili, la kwanza la nchi sita lakini na bomba jipya la nchi 10,”amesema.

Amefafanua faida nyingine ya kukamilika kwa bomba hiloni endapo kutakuwa kunahitajika kufanyika matenegezo watakuwa wanatumia bomba mojawapo wakati lingine likiendelea kufanyiwa matengenezo.

Aidha amesema mardi huo ulianza kujengwa Desemba 5 mwaka 2022 kwa hiyo kwa namna moja au nyingine mradi huo umekamilika ndani ya miezi sita na jumla ya urefu wa bomba hilo kilometa 2.8 ambapo ndani yake mita 960 limepita baharini kwenda Kigamboni .

Kwa upande wake Meneja wa Oryx Gas Tanzania Peter Ndomba amefafanua jitihaza za kuboresha miundombinu ya Oryx ukiwemo ujenzi wa bomba hilo unatokana na ajenda ya Serikali ya kutaka angalau kwa miaka 10 ijayo watumiaji wa nishati safi ya kupikia itoke asilimia tano mpaka kufikia asilimia 80.

“Na ndani ya mwaka mmoja taasisi zote kubwa zihamie kwenye nishati safi ya kupikia, sasa tunaposema nishati safi ya kupikia maana yake lazima hata sisi wadau tuongeze uwezo wa kufikisha hizo gesi mpaka vijijini.

“Kumbuka zamani tulikuwa na uwezo wa kupokea gesi kidogo , kwa hiyo labda ilikuwa na changamoto kubwa sana kusambaza gesi kwa wingi sehemu zote za Tanzania, lakini sasa hivi tumeongeza uwezo wa bomba na tunaongeza tanki kubwa muda si mrefu,”amesema.

Ndomba amesema kwa sasa watakuwa na nafasi ya kuhudumia jamii kubwa ya Watanzania inayokadiriwa kufikia zaidi ya milioni 61 kwa muda mfupi na kwa haraka na hivyo kukidhi hitaji la huduma za nishati safi ya kupikia kwa watu wote.

 

“Tunapokuja kufanya juhudi kama hizi ni mabilioni ya fedha yanatumika kwenye kujenga miundombinu na juhudi kama hizi zinapofanyika hata mwananchi anapoona inamfanya ambavyo Oryx Gas imedhamiria kubadilisha maisha ya watu.Zaidi ya hapo tumekuwa tukigawa mitungi kwenye taasisi na makundi mbalimbali ya wananchi .

“Katika kipindi cha mwaka mmoja tumegawa mitungi ya gesi na majiko yake zaidi 7000 na lengo la kufanya hivyo ni kuonesha mfano kwamba huu ni wakati mabadiliko, sio muda wa kuendelea kutumia kuni na mkaa,”amesema.

 

Wakati huo huo Antigon Kavishe ambaye ni Meneja Oryx Gasi Tanzania -Kigamboni amesema lengo kuu la ujenzi wa bomba hilo ni kupunguza muda wa kupokea gesi kutoka kwenye meli na hivyo kufanya nishati hiyo kupatikana wakati wote na katika maeneo yote.

Previous articleBINTI ALIYETOWEKA SIKU 36 APATIKANA KWA MUUZA MKAA_ MAGAZETINI LEO JUMAMOSI JUNI 24/2023
Next articleSEKTA YA MADINI KUONGEZA MCHANGO WAKE KWENYE PATO LA TAIFA MWAKA WA FEDHA 2023/24

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here