Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora
(THBUB) imetoa taarifa kwa vyombo vya Habari kuhusiana na kifo cha aliyekuwa Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Marehemu Nusura Hassan Abdallah, ambacho chanzo chake kilizua mkanganyiko, ambapo baadhi ya watu walikihusisha na ajali ya gari iliyomhusu Mhe. Dkt. Festo John Dugange, Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa – OR, TAMISEMI (Afya) na kubainisha kuwa vipimo vilivyofanywa na Hospitali ya Faraja iliyopo Mkoani Kilimanjaro vilionesha kuwa kifo cha mwanafunzi huyo kilitokana na shambulio kali la kupanda kwa sukari na upungufu wa damu.
Taarifa Hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji Mstaafu Mathew P. Mwaimu June 2, 2023 Jijini Dodoma huku akitoa wito kwa Jeshi la Polisi na Mamlaka nyingine kuchukua atua ili kuwabaini wale wote wanaohusika na kutoa taarifa za uongo na chonganishi zinazosababisha taharuki katika jamii.
Aidha, amelitaka Jeshi la Polisi Tanzania kwa kushirikiana na mamlaka za usafiri barabarani liweke vifaa vya kiusalama barabarani kama vile kamera ili kubaini (detect) matukio yanayotokea barabarani.
”Jeshi la Polisi Tanzania kwa kushirikiana na mamlaka za usafiri barabarani liweke vifaa vya kiusalama barabarani kama vile kamera ili kubaini (detect) matukio yanayotokea barabarani”amesema Jaji Mathew Mwaimu.
Hata hivyo amewataka wananchi kuwa na amani na vyombo vya Dola katika kuzuia na kupambana na uhalifu na kutoa ushirikiano katika kuvisaidia vyombo hivyo kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.