Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan ametoa wito Kwa Watanzania kutokubali mtu yeyote au kikundi cha watu kuwagawa Kwa kisingizio chochote kile na kudai Tanzania ni Moja na kamwe haitokugawanyika.
Pia ametoa wito kwa watanzania kuwaenzi mashujaa wetu wote kwa kudumisha amani ,umoja ,mshikamano na utulivu na kufanya kazi kwa bidii ili kuleta maendeleo Kwa Taifa letu.
Rais Dkt.Samia ameyasema hayo julai 25, 2023 Jijini Dodoma wakati akiweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa mnara wa kumbukumbu ya mashujaa unaojengwa katika Mji wa Mtumba Dodoma ikiwa ni maadhimisho ya siku ya kumbukumbu ya mashujaa,shughuli iliyoambatana na kuweka mchanga wa ujenzi, kusaini kitabu maalum cha maombelezo ya mashujaa na kupigwa kwa mizinga miwili, ambapo kulifuatia hali ya ukimya kwa dakika moja.
“Kukamilika kwa uwanja huo wa mashujaa utaendelea kuongeza heshima na hadhi ya makao makuu yetu ya nchi hivyo nirejee kuwashukuru ofisi ya Waziri Mkuu, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa pamoja na majeshi yetu kwa maadalizi mazuri ya maadhimisho haya na kusimamia vizuri awamu ya kwanza ya ujenzi wa awamu hii na mnara na sasa wa ujenzi unaoendelea wa mnara wa kudumu kwasababu nimeambiwa mnara uliopo hapa ni mnara wa mwaka huu tuu pengine mwakani nitakuja kwenye mnara wa kudumu ambao ujenzi wake unaendelea”_Amesema Rais Dk.Samia.
“Nilipofika nilionyeshwa ramani ya namna ya uwanja huu utakavyokua nimevutiwa sana na ramani ya uwanja wa mashujaa ,uwanja huu utakua na migahawa ya kimataifa ,utakua na kumbi za mikutano, utakua na vivutio vingine vya watu kupumzika na kupata burudani kama michoro ilivyoonyesha kubwa zaidi zaidi utakua na mnara mrefu kabisa ndani ya Afrika yetu kabla ujengwe mwingine kabla wetu haujakamilika lakini kama wetu utakamilika mwanzo utakua na sifa hizo za kuwa mnara mrefu kabisa ndani ya Afrika ,” amesema Rais Dk. Samia
Hata hivyo ameielekeza ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na ofisi zingine kuendelea kusimamia kwa karibu ujenzi wa mnara pamoja na ujenzi wa uwanja wa mashujaa pamoja na miundombinu mingine ,yote ikamilike kwa wakati na kwa viwango viliovyokusudiwa.
“Vilevile wizara ya fedha ihakikishe kwamba inatoa fedha kwakuzingati mpangokazi wa ujenzi huu na kusiwe na ucheleweshwaji wowote,” ameongezea Rais Dk. Samia.