Mkuu wa mkoa wa Njombe Anthony Mtaka amesema Tanzania ina watu walio changanyikiwa (Wehuka) kwasababu ya kupata fedha nyingi na za ghafla kutokana na fidia ya maeneo wakati wa kupisha miradi mikubwa ikiwemo ya madini.
Mtaka amebainisha hayo wilayani Ludewa wakati akizungumza na wananchi wa kata ya Nkomang’ombe juu ya fedha nyingi za fidia zinazokwenda kulipwa kwa wanaopisha mradi wa madini ya makaa ya mawe na madini mengine katika mradi wa Mchuchuma.
“Tumekuja kuzungumza na watu wa Nkomang’ombe kwamba zinakuja fedha,tunao watu Tanzania wamebadilisha maisha kwasababu ya fidia ya maeneo yao na tunao watu pia ambao wameheuka kwasabu ya fedha hizi za fidia”amesema Mtaka
Aidha Mtaka katika mkutano huo amemuagiza mkuu wa wilaya ya Ludewa Victoria Mwanziva kuhakikisha wataalamu wa halmashauri hiyo wanapima mji na viwanja kwenye kata hiyo ili kuendana na mabadiriko yanayokwenda kutokea baada ya mradi kuanza.
Katika kata ya Nkomang’ombe takribani wananchi 650 wanatarajia kunufaika na fedha kiasi cha shilingi Bilioni 5.2 zilizotolewa na serikali kwa ajili ya malipo ya fidia yao baada ya kupisha mradi.