Home KITAIFA “TANZANIA IMEFANIKIWA KUTOKOMEZA MARBURG KUTOKANA NA UONGOZI MAHIRI WA RAIS SAMIA”- UMMY

“TANZANIA IMEFANIKIWA KUTOKOMEZA MARBURG KUTOKANA NA UONGOZI MAHIRI WA RAIS SAMIA”- UMMY

 

Na WAF, Gaborone – Botswana

Tanzania imefanikiwa kukabiliana na kutokomeza Ugonjwa wa Marburg ambao ulitokea katika Mkoa wa Kagera ndani ya siku 78 tu Sababu kubwa zilizofanikisha mapambano hayo yalitokana na utashi wa kisiasa na uongozi thabiti toka kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu ameyasema hayo leo Agosti 31, 2023 wakati akishiriki Kikao cha kusherehekea Mwaka mmoja wa Bara la Afrika katika kutekeleza malengo ya Usalama wa Afya.

“Chini ya uongozi mahiri wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan tulifanikiwa kuutokomeza ugonjwa wa Marburg ndani ya siku 78 tu uliotokea katika Wilaya ya Bukoba Mkoani Kagera”, amesema Waziri Ummy

Kikao hicho cha kusherehekea Mwaka mmoja wa Bara la Afrika katika kutekeleza malengo ya Usalama wa Afya kimefanyika pembezoni mwa Mkutano wa 73 wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Àfrika Mjini Gaborone, Botswana.

Aidha, Waziri Ummy wakati akiongea katika Mjadala huo wa wazi ameelezea utayari wa jamii katika kutoa taarifa za haraka kwenye ngazi husika za Afya, uwepo wa wataalam waliopata mafunzo na kutayarishwa kwa usahihi kuhusu udhibiti wa Magonjwa ya milipuko, utayari wa wataalam katika kukabiliana na magonjwa mbalimbali pamoja na ushirikishwaji wa karibu wa wadau wa Sekta ya Afya.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika, Dkt. Moeti ameelezea jinsi WHO Kànda ya Afrika ilishirikiana na nchi mbalimbali katika kukabiliana na milipuko ya magonjwa kama Kipindupindu katika nchi za Msumbiji na Afrika Kusini.

“Pia, katika ushirika huo tuliofanya umesaidia kufanikisha kikamilifu katika kusaidia wakimbizi kutokana na vita ya wenyewe kwa wenyewe katika Nchi ya Sudan ambayo ilikuwa inatishia milipuko ya magonjwa kwenye makambi Nchini Chad”, amesema Dkt. Moeti

Mwisho, Dkt. Moeti amezishukuru na kuziomba nchi wanachama kuhakikisha kuwa zinatoa kipaumbele katika kukabiliana na milipuko ya magonjwa kwa wakati ili kuwahi kukabiliana na magonjwa hayo.

Washiriki wa mkutano huo wakupongeza juhudi na umahiri wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kudhibiti, kuzuia na hatimae kutokomeza kabisa ugonjwa wa Marburg na kufanya Nchi, Bara la Afrika na Dunia kuwa salama.

Mkutano huo umekubaliana umuhimu wa kuwa na wataalaam katika ufuatiliaji wa magonjwa katika Bara la Afrika na hususani kuhakikisha mifumo ya utawala na huduma inafanya kazi kwa wakati na haraka.

Previous articleWAWILI AKIWEMO MCHUNGAJI WASHIKILIWA NA POLISI KWA KULAGHAI MCHAWI KADONDOKA NA UNGO KANISANI KWENYE MKESHA
Next articleSERIKALI YAPIGA MARUFUKU KUTUMA NYARAKA ZAKE KWA NJIA YA WHATSAPP

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here