Home KITAIFA TANROADS NI BANDIKA BANDUA KATIKA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA UJENZI WA MIUNDOMBINU...

TANROADS NI BANDIKA BANDUA KATIKA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA UJENZI WA MIUNDOMBINU MOROGORO

 

Meneja wa TANROADS Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Alinanuswe Kyamba akiongea na waandishi wa habari mjini Morogoro Aprili 15, 2023 akielezea utekelezaji wa miradi mbalimbali inayotekelezwa na TANROADS katika Mkoa wa Morogoro
Meneja Mwandamizi, Msimamizi wa Kitengo cha Ununuzi na Ugavi TANROADS-Morogoro, Mhandisi Mussa Kaswahili akiongea na waandishi wa habari Aprili 15, 2023 wakati wa ukaguzi wa miradi inayotekelezwa na Wakala Wa Barabara Tanzania (TANROADS) katika Mkoa wa Morogoro

Na Mwandishi Wetu Morogoro

Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) umetekeleza miradi mbalimbali ya ujenzi wa miundombinu ikiwemo madaraja na barabara mkoani Morogoro jambo ambalo limepelekea kufungua fursa za kiuchumi kwa wananchi wanaoishi maeneo ambayo miundombinu hiyo imejengwa.

Mikoa wa Morogoro umebahatika kuwa na miradi mingi ya ujenzi wa miundombinu ambapo katika miradi miwili iliyopo mmoja tayari umeshakamilika.

Hayo yamesemwa Aprili 15, 2023 na Meneja wa TANROADS Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Alinanuswe Lazeck Kyamba akiongea wakati wa kutembelea na kukagua maendeleo ya miradi ya ujenzi wa miundombinu katika wilaya za Kilosa na Kilombero mkoani humo ambapo amesema mbali na miradi hiyo miwili kuna miradi mingine mitano ambayo tayari fedha zake zimeshatolewa.

“Mwaka jana Mhe. Rais ametoa fedha za kutekeleza miradi mingine mitano ambayo utekelezaji wake unaanza mwaka huu, zabuni za miradi hiyo zimeshafunguliwa kwa sasa tunatafuta mkandarasi mwenye sifa ya kutekeleza miradi hiyo” alisema Mhandisi Kyamba

Akizungumzia miradi iliyokamilika, Mhandisi Kyamba ameitaja miradi hiyo kuwa ni pamoja na mradi wa kurekebisha maeneo korofi (black spots) katika maeneo ya Kingolwira, Iyovi na Mikumi lengo likiwa ni kutokomeza kabisa ajali zinatokoea mara kwa mara katika maeneo hayo.

Mhandisi Kyamba ameendelea kwa kusema kuwa, TANROADS inaendelea na utekelezaji wa mradi wa Ludewa hadi Kilosa ambao upo katika hatua za mwisho kukamilika.

Kuhusu utekelezaji wa mradi wa Kidatu-Ifakara unaogharimu kiasi cha shilingi Bilioni 105, Mhandisi Kyamba amesema

“Utekelezaji wa mradi wa kidato-Ifakara umefikia asilimia 78, mradi huu unahusisha ujenzi wa daraja la Ruaha Mkuu ambapo daraja la zamani lilikuwa lina uwezo wa gari moja kupishana lakini daraja jipya litakuwa na uwezo wa kuruhusu magari mawili kupishana”

Katika hatua nyingine Mhandisi Mwandamizi, Msimamizi wa Kitengo cha Ununuzi na Ugavi, TANROADS Morogoro,
Mhandisi Mussa Madirisha Kaswahili ameishukuru serikali ya awamu sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutenga fedha na kuendelea kupeleka fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali mkoani Morogoro ikiwemo ujenzi wa daraja la Ruaha Mkuu, daraja ambalo amelitaja kama kichocheo cha uchumi hususan kwa wakazi wa Morogoro ambako barabara ya Morogoro hadi Ifakara inapita .

Akigusia mradi wa maboresho na upanuzi wa mzani wa Mikumi Mhandisi Kaswahili ameeeleza kuwa, eneo la mizani lilikuwa na changamoto mbalimbali zilizopelekea huduma ya upimaji kuchukua muda huku changamoto za usumbufu na msongamano wa magari zikiwa ni kikwazo kikubwa katika utoaji wa huduma za upimaji.

Mwonekano wa maendeleo ya kazi katika mradi wa maboresho na upanuzi wa mzani wa Mikumi

“Eneo la mizani Mikumi awali lilikuwa na mzani mmoja na mzani huo ulikuwa unapima magari uelekeo wa Morogoro ambapo kulikuwa na msongamano mkubwa wa magari wakati wa upimaji. Serikali ikatenga fedha kwa ajili ya kuboresha mzani huu kwa kuongeza mzani uelekeo wa Iringa” alisisitiza Mhandisi Kaswahili na kuongeza kuwa

“Awali magari yote tulikuwa tunayapima kwa magari hayo kuingia eneo la mzani lakini kwa maboresho yanayoyafanyika tutaweka WIM (Mzani unaopima magari yakiwa kwenye mwendo) na kufanya magari yenye uzito wa wastani kutokuwa na ulazima wa kuingia katika mizani lakini yatakayooneshwa yanahitaji kupimwa yataingia kwenye mizani”

Maboresho kama hayo ya mizani yanafanyika pia katika mzani wa Mikese ambapo Mhandisi Kaswahili amesema

“Mzani wa Mikese nao utaongezewa WIM upande wa kuelekea Dar es Salaam pamoja na mzani ambao utawezesha kupima magari kwa mitaimbo yote kwa pamoja, tofauti na sasa ambapo unapima kwa mtaimbo mmoja mmoja. Maboresho haya yatakwenda kuondoa changamoto ya msongamano wa malori katika eneo la Mikese”

Wakiongea kwa nyakati tofauti madareva wanaotumia barabara ya Kidatu hadi Ifakara, kwa niaba yao Ally Namulisa amesema, wamesema awali walikuwa wanapata changamoto ya ubovu wa barabara hiyo kuwa na mashimo na kupelekea wakati mwingine kulala njiani hususan nyakati za mvua na kuchukua masaa mengi kutoka Ifakara kwenda Kidatu au Ifakara kwenda mikoani.

Dereva Ally Namulisa akiongelea namna alivyokuwa anapata changamoto katika shughuli zake kabla ya maboresho yaliyofanywa na ujenzi wa barabara ya Kidatu hadi Ifakara

Wawakilishi wa wananchi mbalimbali wanaoishi katika maeneo ambayo barabara ya Kidatu-Ifakara inapita wakiongozwa na diwani kata ya Mwaya wilayani Kilombero, Mheshimiwa Antony Mwampunga wameeleza kuwa, kukamilika kwa barabara hiyo kuwa ni ukombozi kwa katika nyanja mbalimbali ikiwemo kiuchumi na kijamii na kugusia kuwa hapo awali nauli zilikuwa juu na abiria kuwa njiani lakini sasa wameweza kufungua biashara mbalimbali pembezoni mwa barabara hiyo kama fursa ya kiuchumi.

Diwani wa kata ya Mwaya wilayani Kilombero, Anthony Mwampunga akielezea manufaa wanayoyapata wananchi mara baada ya ujenzi wa barabara ya Kidatu-Ifakara
Mwonekano wa barabara ya Kidatu-Ifakara
Kazi mbalimbali za ujenzi wa daraja jipya la Ruaha Mkuu zikiwa zinaendelea, kama zilivyokutwa na mpiga picha Wetu

Serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi kugharamia ujenzi wa barabara katika
maeneo mbalimbali ya nchi.
TANROADS Mkoa wa Morogoro imefafanua kuwa, uwepo wa mizani bora ndani ya mkoa wa Morogoro na nchi kwa ujumla ni moja ya mikakati waliyokuwa nayo kuhakikisha barabara zinazojengwa kwa gharama kubwa zinadumu
na kuwa magari yanayopita katika barabara yana uzito unaotakiwa.

Previous articleMWONEKANO MPYA NGORONGORO
Next articleMATAJIRI WAHUSISHWA UFUKUAJI WA MAKABURI MANYONI-SINGIDA_MAGAZETINI LEO JUMATATU APRILI 17/2023

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here