Home KITAIFA STAKABADHI GHALANI ZAIPA SERIKALI MIL.170 , WAKULIMA WASHUKURU

STAKABADHI GHALANI ZAIPA SERIKALI MIL.170 , WAKULIMA WASHUKURU

 

NA JOSEA SINKALA, MAGAMBA SONGWE.

Zaidi ya tani 1500 za zao la Ufuta zimeuzwa na Serikali wilayani Songwe hivyo kuipatia fedha zaidi ya Sh.Million 170 kupitia mfumo wa Stakabadhi ghalani ambao umeendelea kutumiwa na wakulima wilayani humo na kuchochea bei ya zao hilo tofauti na miaka ya nyuma.

 

Hayo yamejiri kufuatia mnada wa zao la ufuta iliyofanyika katika Kata ya Magamba Wilayani Songwe ambapo kampuni 17 zilijitokeza kila mmoja akitangaza bei ya kununua zao hilo kupitia mfumo wa Stakabadhi ghalani.

 

Hata hivyo Wakulima kutoka maeneo mbalimbali Wilayani Songwe wameishukuru Serikali kusimama kidete kuhakikisha mkulima hanyonywi kwa maendeleo endelevu.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Songwe Cessilia Kavishe amesema mfumo huo unatajwa na Halmshauri ya Songwe kuwa ni mzuri tofauti na hapo awali ambapo inadaiwa kuwa baadhi ya wafanyabiashara walikuwa wakiwalaghai wakulima kwa kuwashinikiza kutouza mazao kwa njia ya stakabadhi ghalani lakini tabia hiyo imepigwa marufuku na wananchi wameendelea kuelimishwa.

 

“Kwa hiyo unaweza kuona kwamba mfumo wa Stakabadhi ghalani sio tu mkulima anayefaidika hata wale ambao hawajalima wanafaidika lakini pia kwa upande wa Halmashauri kila tunapouza tunatengeneza pesa kupitia ushuru moja kwa moja kuliko ule ambao tulikuwa tunatumia nguvu kubwa sana ambao pia ulikuwa unatengeneza madeni kwenye POSI zetu (Mashine za kukusanyia ushuru)”, Mkurugenzi Halmashauri ya Songwe CPA Cessilia Kavishe.

“Sasa hivi ni kwamba mfanyabiashara moja kwa moja anatulipa sisi (Serikali), tukichukulia mfano tu kwenye mnada huu wa sasa tunaenda kupokea zaidi ya Million 170”, Mkurugenzi Halmashauri ya Songwe CPA Cessilia Kavishe akizungumza na Jambo Tv baada ya Mnada wa zao la Ufuta Wilayani Songwe.

 

Aidha Mkurugenzi wa Halmashauri ya Songwe CPA Cessilia Kavishe, amesema Serikali wilayani humo (Songwe) imepanga kujenga maghala makubwa mawili kwa ajili ya kuhifadhia zao la ufuta katika kudumisha utamaduni wa wakulima kuuzia mazao yao stakabadhi ghalani.

Mrajisi msaidizi wa Tume ya maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) Mkoa wa Songwe Benjamin Mwangwala amesema dhamira ya Serikali ni kuona mkulima anauza mazao yake kwa faida huku Serikali ikipata gawio lake kupitia ushuru kwa maendeleo endelevu ya Taifa. Pia amewataka wakulima kuendelea kutumia mfumo wa stakabadhi ghalani.

 

Mwenyekiti wa Chama kikuu cha Ushirika mkoa wa Songwe Soreco amesema Mkoa unaendelea kushirikiana kuhakikisha wanakuwa daraja kati ya wakulima na wanunuzi.

Taasisi ya Tume ya maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) inafanya kazi chini ya Wizara ya Kilimo ikiwa lengo lake kuu ni kuhakikisha inasajili, inasimamia na kudhibiti Vyama vya Ushirika nchinu kufanya kazi yake ipasavyo kwa mujibu wa sheria namba 6 ya 2013.

Previous articleDKT. SLAA AANIKA ANAVYOTETA NA MBOWE , LISSU _ MAGAZETINI LEO ALHAMISI MEI 25/2023
Next articleMTOTO WA TEMBO ALIYETUMBUKIA KISIMANI AOKOLEWA

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here