NA JOSEA SINKALA, SONGWE.
Mkuu wa Mkoa wa Songwe Dkt. Francis Michael, ameziagiza Halmashauri zote za Mkoa huo kutumia vizuri fedha zilizotolewa na Serikali ya awamu sita kwa ajili ya mradi wa BOOST kwa lengo la kuboresha miundombinu ya Shule za msingi.
Hata hivyo, Dkt. Michael amezionya Halmashauri hizo kutumia fedha hizo za BOOST bila kuongeza fedha yeyote kutoka kwenye mapato ya vyanzo vya ndani (Own source).
Amesema Serikali imetoa kiasi cha shilingi bilioni 7,138,500,000 kwa ajili ya ujenzi miundombinu wa Shule za msingi 8 mpya, vyumba vya madarasa 104, pamoja na vyumba vya madarasa ya mfano kwa ajili ya elimu ya awali vyumba 10.
Pia fedha hizo zitahusika katika ujenzi wa vyumba vya madarasa 2 kwa ajili wanafunzi wenye mahitaji maalumu, matundu ya vyoo 104 na Nyumba za waalimu 2 ambazo zitachukua familia 4.
“Matarajio ya Serikali ni kuona fedha iliyokuja inakwenda kukamilisha miradi yote kwa wakati ili iendelee kuleta fedha nyingine za ujenzi wa miundombinu, kwani fedha izi ni za lipa kwa matokeo (P for R) jinsi unavyotumia vizuri ndio Serikali inakuongezea fedha kupitia mradi wa BOOST amesisitiza, Mhe. Dkt. Francis Michael.
“Serikali imeshatoa maelekezo kuwa ifikapo 30 Juni miradi yote iwe imekwisha lakini sisi hapa Mkoani tunataka kuona miradi yote ya BOOST inakamilika ifikapo 15 Juni bila kuongeza fedha yeyote kutoka mapato ya ndani” amesisitiza Mhe. Dkt. Francis Michael.
Ametaja kiasi cha fedha kwa kila Halmashauri kuwa Ileje imepata kiasi cha shilingi 1,574,100,000, Mbozi shilingi 1,700,100,000, Momba shilingi 1,114,600,000, wakati Halmashauri ya Songwe shilingi 1,039,600,000 na Tunduma TC 1,707,1000,000.
Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule ya msingi Mlowo Mwl. Denis Jimy, ameishukuru Serikali kwa kupata mradi wa BOOST kwa ajili ya Kitengo cha elimu maalumu ambacho kina wanafunzi 75, amesema wamepata fedha milioni 50 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba 2 vya madarasa kwa ajili ya elimu maalumu na milioni 6 kwa ajili ya kujenga matundu 3 ya vyoo.