Leo Mei 23, Nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa wanaadhimisha siku ya kimataifa ya kutokomeza ugonjwa wa Fistula au Nasuri, unaowapata wanawake baada ya kujifungua.
Kulingana na takwimu za Shirika la afya duniani kila mwaka wanawake zaidi ya laki tano kwenye mataifa yanayoendelea huugua Fistula kutokana na uzazi wenye hitilafu.
Baada ya kubainika kuwa ugonjwa huo unaweza kuepukwa, wadau na wataalamu wa afya duniani, wanalenga kuhakikisha kuwa hakuna tena Fistula duniani kufikia mwaka 2030.
Umoja wa Mataifa unasema hilo litawezekana tu ikiwa ufadhili wa kutosha utatolewa kuwezesha kuwepo kwa mifumo thabiti ya afya ya uzazi.
Zaidi ni kwamba jamii inamsaidia Mama mjazito kufika kwenye kituo cha afya ili aweze kujifungua salama. Wakati huohuo, wasichana wanahimizwa kujiepusha na mimba za utotoni kwani hawajakomaa kuweza kujifungua salama.
Ugonjwa wa Fistula ya uzazi huwapata wanawake wakati wa kujifungua hasa wale wanaojifungua wakiwa na umri mdogo pamoja na kukosa msaada stahiki wakati wa kujifungua.