NA JOSEA SINKALA, MOMBA SONGWE.
Mjumbe wa Kamati ya Sera na Utafiti wa CHADEMA Kanda ya Nyasa na mtia nia ya Ubunge Jimbo la Momba mkoani Songwe (2020) Gideon Siame, amesema ikiwa Serikali imeamua kutoa ruzuku ya Mbolea kwenye Kilimo lazima ihakikishe wakulima wanafikiwa na Mbolea hizo kwa wakati na zenye kutosheleza ili wananchi walime kwa tija licha ya bajeti ndogo aliyodai kuidhinishwa na Bunge la Tanzania.
Siame ambaye pia alikuwa mtia nia ya Ubunge jimbo la Momba kupitia CHADEMA amesema hayo alipokuwa mgeni rasmi kwenye Sikukuu ya Wanawake Kanisa la African Church Mission of Tanzania Ushirika wa Nakawale kata ya Ikana Wilayani Momba.
Siame, ameitaka Serikali kupitia Wizara ya Ardhi kutoa bei elekezi ya urasimishaji Ardhi kutokana na kuwepo kwa baadhi ya watu wanaopima ardhi kujipangia bei hali inayomuumiza mwananchi.
“Ni vizuri sasa Serikali itoke hadharani na kusema kwamba tunapotaka kurasimisha ardhi zetu inabidi tuwe na shilingi ngapi maana leo hii ni kizungumkuti yaani kila mtu akija kwamba anarasimisha ardhi kila mmoja ana bei yake, hili sio zuri hata kidogo. Lakini pia niwaombe wananchi wa Nakawale, Ikana, Momba na sisi sote tujitahidi tuhakikishe tunarasimisha ardhi zetu ili kukopesheka na taaisisi za kifedha na kuinua uchumi wetu ikizingatiwa baadhi yetu maeneo yetu ni viwanja sio mashamba tena”, Gideon Siame, Mtia nia Ubunge jimbo la Momba kupitia CHADEMA (2020).
Pia amesema ikiwa Serikali imeamua kutoa ruzuku ya mbolea ihakikishe wakulima wanafikiwa na mbolea hizo kwa wakati na zenye kutosheleza ili wananchi walime kwa tija.
Pia amewahimiza wananchi wa Kijiji cha Nakawale na Momba kwa ujumla kurasimisha ardhi zao ili kulinda raslimali hiyo kwa manufaa ya vizazi vijavyo kiuchumi na kijamii ikizingatiwa Wilaya hiyo ni wazalishaji wakubwa wa mazao mbalimbali hasa ya Chakula ikiwemo Mahindi, Maharage, ufuta na mpunga.
Sambamba na hilo kwenye sikukuu hiyo iliyohusisha harambee ya kutunisha mfuko wa wanawake hao, Gideon Siame amechangia Fedha kiasi cha shilingi laki tatu (Tsh. 300,000/=) kwa ajili ya kutunisha mfuko wa wanawake hao ambao lengo lao kubwa ni kuanzisha mradi wa Shamba ili kujiinua kiuchumi.
Katika harambee hiyo Umoja wa Wanawake wa Kanisa la African Ushirika wa Nakawale Momba mkoani Songwe wamepata fedha zadi ya Shilingi laki tisa.