Halmashauri ya wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro imesema shule za Msingi za serikali 190 kati ya 229 zinakabiliwa na uchakavu wa miundombinu katika hali tofauti hivyo kutakiwa kufanyiwa ukarabati au kujengwa upya.
Hayo yameelezwa na Afisa Elimu Msingi na Awali wilayani humo, Gaudence Assey wakati wakupokea misaada mbalimbali ikiwemo makabidhiano ya choo cha kisasa cha wanafunzi wa shule ya Msingi Mkolowonyi kilichojengwa na Shirika lisilokuwa la kiserikali la Rawuya Foundation na kuongeza kuwa hali hiyo ya uchakavu imetokana na miundombinu ya shule hizo kujengwa katika miaka ya 1940 na bila kufanyiwa ukarabati.
Assey amesema shule nyingi zilijengwa na wazazi ambapo uchakavu wake ni mkubwa licha ya kuwa hakuna shule ambayo imezuiliwa kuendelea kufundisha kutokana na uchakavu huku Vyoo vingi vilijengwa juu ya mashimo hali inayopelekea kuhatarisha usalama wa wanafunzi walioko shuleni hivyo halmashauri imekuwa ikiendelea kukarabati kidogo kidogo kulingana na bajeti inayoipata.
Awali akitoa taarifa ya shule, Mwalimu Mkuu wa Shule ya msingi Mkolowonyi Agustina Moshy ameleeza kuwa shule hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa vyoo kwaajili ya walimu,uchakavu wa majengo ya shule na Ofisi ya Walimu na Mwalimu mkuu hali inayo athiri ufundishaji na ujifunzaji hasa wakati wa mvua pamoja na uhaba wa walimu.
“Uchakavu wa majengo ya shule unatishia usalama wetu hapa shuleni pamoja na uhaba wa walimu kwani tupo walimu sita na uhitaji ni walimu tisa hivyo walimu kuwa na mlundikano wa vipindi vingi, ukosefu wa maktaba,bwalo la chakula na ukosefu wa huduma ya maji vinatuathiri kwakweli” alisema Moshy.
Akitoa taarifa ya kazi zilizo fanywa na shirika hilo la Rawuya Foundation Mwenyekiti wa shirika hilo Emmanuel Kimei ameeleza kuwa shirika hilo linalenga kusaidia Jamii katika kuwakuza kielimu,kiafya na utamaduni na shirika hilo litatoa misaada Tanzani nzima.
Kimei ameeleza kuwa shirika hilo kupitia wadau waliosoma katika shule ya Msingi Mkolowonyi wamefanikiwa kujenga choo cha kisasa cha Wanafunzi chenye matundu tisa,kutoa chakula ikiwemo mahindi na maharage kwa wanafunzi,taulo za kike pamoja na kuanza kukusanya fedha za kukarabati madarasa ya shule hizo.
“Shule ilikaribia kufungwa baada ya wanafunzi kukosa choo tumefanikiwa kujenga choo cha kisasa kilicho gharimu milioni 25,tunataka kuona shule inaboreshwa na wanafunzi wanapata elimu katika mazingiraa rafiki pamoja na walimu wao,aidha tunafanya mpango wa kukarabati mifereji ya maji ili itumike katika ufugaji wa samaki na kilimo cha umwagiliaji” alisema Kimei.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Mamba Kusini Elirehema Tesha akimwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Moshi amepongeza shirika hilo kwa kuanza kutengeneza mazingira ya nyumbani na kutoka nje kwenda kwa watanzania wote hasa kwa kutambuaa umuhimu wa elimu.
“Choo kilicho kuwepo hapa kilikuwa ni shida na ilikuwa rahisi watoto kupata magonjwa ya mlipuko,shirika limeokoa afya za watoto na wananchi kwa ujumla endeleeni kupenyeza na kusaidia jamii ya watanzania wote” alisisitiza Tesha.
Aidha katika kuunga mkono jitihada za ukarabari wa majengo ya shule hiyo Diwani huyo amechangia mabati matano huku akiahidi kupatikana kwa Shilingi milioni tatu katika mfuko wa maendeleo ya kata zitakazo saidia kukarabati shule hiyo.