Home KITAIFA SHILINGI BILIONI 25 ZATENGWA MAPAMBANO DHIDI YA UKIMWI

SHILINGI BILIONI 25 ZATENGWA MAPAMBANO DHIDI YA UKIMWI

NA MWANDISHI WETU- NJOMBE

Serikali kupitia tume ya kudhibiti UKIMWI, TACAIDS imeongeza bajeti ya mapambano dhidi ya UKIMWI kutoka shilingi bilioni 14 katika mwaka wa fedha ulioisha hadi bilioni 25 katika mwaka mpya wa fedha 2023/2024 ili watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI waweze kupata dawa kwa uhakika na kuendeleza shughuli zao.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri Ofisi Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga, alipowatembelea watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI katika Halmashauri ya Mji wa Njombe ambapo alisema lengo la Serikali ni kuona WAVIU wanaendelea vyema na maisha yao huku wito ukitolewa kwa wanaume kujiunga kwenye vikundi pindi wanapobainika kuwa na maambukizi.

Pia alipongeza hatua ya uanzishwaji wa Konga katika kila Kata akisema hatua hiyo huwaleta pamoja kw akushirikiana katika shughuli za uzalishaji na kujiona ni sehemu ya nguvu kazi ya Taifa.

“Niupongeze Mkoa wa Njombe mmepiga hatua kubwa sana katika mapambano dhidi ya UKIMWI,kuanzishwa kwa Konga hizi katika kila Kata inaleta faraja kwa WAVIU kwani wanapata fursa ya kujadili mambo yao na kufanyiwa kazi ,”Alisema Mhe. Ummy.

Vilevile Mhe. Ummy alibainisha kwamba Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Mheshimiwa, Dkt. Samia Suluhu Hassan imejidhatiti kuhakikisha wananchi wake wanaimarika kiuchumi hivyo akawahimiza WAVIU kujitokeza kwa wingi kuchukua mikopo ili kuboresha shughuli zao.

Katika hatua nyingine aliwahimiza wanaume kujitokeza kwa wingi kupima afya zao na kujitambua mapema hali zao na kuanza mara moja matumizi ya dawa za kufubaza virusi vya UKIMWI

“Kwa mujibu wa takwimu inaonyesha watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI kwa Mkoa wa Njombe ni zaidi ya 63,000 huku wanaume takribani 31,372 kwa Mkoa mzima wamepima afya zao nitumie nafasi hii kupongeza konga zetu na wadau wa maendeleo wakiwemo NACOPHA pamoja na hamasa kubwa iliyotolewa na Mhe. Kassim Majaliwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,”Alibainisha.

Aidha aliwasisitiza kutosita kujitokeza kuchukua mkopo wa asilimia 10 ambao hutolewa na Serikali kupitia Halmashauri pindi mfumo huo wa mikopo utakaporejeshwa tena.

Naye Mratibu wa UKIMWI Halmashauri ya Mji wa Njombe Bwa. Daniel Mwasongwe alisema Halmashauri hiyo imefanikiwa kuwafikia wateja wapya 12,717 katika huduma ya upimaji kwa kipindi cha mwezi Januari hadi Machi mwaka huu na kuwaunganisha na Huduma ya Dawa kwa waliokutwa na VVU.

Kwa upande wake Katibu wa Konga Halmashauri ya Mji wa Njombe Bwa. John Msofu na Katibu wa Kikundi cha watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI Kata ya Ramadhani (JIUKU),Bwa. Rajab Safari kwa niaba ya WAVIU wamesema wamekuwa wakiendelea na shughuli mbalimbali za ujasiriamali ikiwemo kilimo cha Parachichi, Mbogamboga na Ufugaji jambo linalowasaidia kupunguza makali ya maisha.

Hata hivyo Halmashauri ya Mji wa Njombe iliomba kutengenezwa kwa mfumo wa Alama za vidole kwa watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI ili kurahisisha changamoto ya kupotea kwa watu wanaotumia dawa.

Previous articleCGP NYAMKA ASISITIZA NIDHAMU KWA MAAFISA NA ASKARI MAGEREZA
Next articlePOLISI ADAIWA KUMUUA KIJANA KWA KUMPIGA RISASI (3) BARABARANI.. NDUGU WAGOMA KUZIKA _ MAGAZETINI LEO JUMAMOSI JULAI 08/2023

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here