Home KITAIFA SERIKALI YATOA MAJIBU KUHUSU UJENZI WA BARABARA YA LAMI MLIMBA

SERIKALI YATOA MAJIBU KUHUSU UJENZI WA BARABARA YA LAMI MLIMBA

 

SERIKALI kupitia kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Godfrey Kasekenya imesema kuwa ni kweli imeshasaini mkataba wa ujenzi wa kiwango cha lami wa Barabara ya kutoka Ifakara hadi Mbingu Mlimba yenye urefu wa km 62.5 na kwamba kinachosubiriwa ni mkandarasi kuanza kazi hiyo.

Naibu Waziri Kasekenya ameyasema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Mlimba, Godwin Kunambi aliyetaka kujua ni lini ujenzi wa barabara hiyo utaanza sambamba na ujenzi wa barabara ya Mafinga hadi Kihansi Mlimba yenye urefu wa km 126.39.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri Kasekenya amesema mkataba baina ya Serikali na Mkandarasi wa ujenzi wa Barabara ya Ifakara hadi Mbingu ulishasainiwa na kinachosubiriwa ni kumalizika kwa siku 28 za Mkandarasi kutoa dhamana ya utendaji kama sheria inavyotaka kisha baada ya hapo ataanza kazi hiyo.

” Ni kweli tumesaini mkataba na mkandarasi na kinachosubiriwa ni yeye atoe dhamana ya utendaji kama sheria inavyotaka kisha ataanza kazi. Na dhamana hiyo anatakiwa aitoe ndani ya siku 28. Lakini pia kuhusu ujenzi wa km 37.5 za kutoka Mbingu hadi Chita ili kukamilisha km 100 nazo muda siyo mrefu tutasaini mkataba na mkandarasi,” Amesema Kasekenya.

Akijibu swali la Mbunge Kunambi kuhusu ujenzi wa barabara ya Mafinga hadi Kihansi Mlimba, Naibu Waziri Kasekenya amesema kiasi cha Sh Milioni 250 kimetengwa kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara hiyo na baada ya kukamilika kwa zoezi hilo na kujua gharama ya ujenzi Serikali itatafuta fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi.

Previous articleREA YAWEZESHA MRADI WA UMEME WA CHANZO CHA MAJI IJANGALA KUINGIA KWENYE GRIDI YA TAIFA
Next articleJADON SANCHO AMJIA JUU KOCHA WAKE KWA KUMUWEKA BENCHI

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here