MKURUGENZI Mtendaji wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo (MOI) Profesa Abel Makubi amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya imetenga jumla ya Sh 55.9 bilioni kwa Taasisi hiyo kwa ajili ya kuboresha huduma za tiba na shughuli za uendeshaji.
Ameyasema hayo leo, Agosti 3, jijini Dodoma wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa Majukumu ya Taasisi hiyo ndani ya miaka miwili ya Serikali ya awamu ya sita na Mipango ya mwaka 2023-2024 kwa waandishi wa Habari katika ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo.
Amesema katika utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2023-2024 Serikali imetenga jumla ya Sh 55.9 bilioni kwa Taasisi hiyo ili kuboresha huduma za tiba na shughuli za uendeshaji
Profesa Makubi ameitaja mipango ya MOI ni pamoja na kuongeza ubora wa huduma zote ndani ili kukidhi matarajio ya wananchi ndani ya nchi na kufikia viwango vya Kimataifa.
Pia,kuanzisha huduma mpya tatu za kibingwa kibobezi ambazo bado zinasababisha rufaa nje nchi (Tiba ya baadhi ya Kiharusi kupitia Angio-suite, Tiba ya baadhi ya vifafa kupitia upasuaji na upasuaji wa kiuno kwa njia ya matundu (Hip arthroscopy).
Ameitaja mipango mingine ni ukarabati wa miundombinu ya Hospitali Ujenzi mpya miundombinu,ujenzi wa jengo jipya la wagonjwa wa nje (OPD) ambalo litakuwa na vyumba 30 vya kliniki vya kisasa tofauti na vyumba 7 vilivyopo sasa.