Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Serikali imetenga kiasi cha shilingi milioni 161 katika bajeti ya mwaka wa fedha 2023/2024 kwa ajili ya kujengea uwezo majukwaa ya uwezeshaji wanawake kiuchumi ambapo kwa Mkoa wa Pwani utakuwa ni miongoni.
Hayo yamesemwa leo Alhamisi Juni 22, 2023 bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wanawake na Makundi Maalum Mhe Mwanaid Khamis akijibu swali la mbunge wa viti maalum Mkoa wa Pwani, Mhe. Subira Mgalu aliyetaka kujua mpango wa serikali katika kuwapa mafunzo majukwaa ya uwezeshaji wanawake kiuchumi ngazi za vitongoji, vijiji, kata na wilaya katika Mkoa wa Pwani.
Akiendelea kujibu swali hilo, Naibu Waziri Mwanaidi ameeleza kuwa, kwa Mkoa wa Pwani pekee umetengewa kiasi cha shilingi milioni 58.5 kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa majukwaa yote yaliyopo mkoani humo na mafunzo hayo yataanza mapema mwaka wa fedha 2023/2024 utakapoanza mwezi Julai, mwaka huu.
Katika kutekeleza hilo, Naibu Waziri Mwanaidi amewaagiza maafisa tawala wa mikoa kote nchini kuandaa program za mafunzo ili pale mwaka wa fedha 2023/2024 unapoanza mafunzo hayo yaanze kutolewa.
Kwa upande wake wake mbunge wa viti maalumu mkoani humo , Subira Mgalu ameishukuru serikali ya awamu sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa hatua hiyo muhimu katika kuwawezesha wanawake katika Mkoa wa Pwani.