Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan ameridhia kutoa kibali cha kuajiri watumishi 21,200 wa Kada za ualimu na Afya.
Hayo yameelezwa leo Aprili 12, 2023 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Angellah Kairuki wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa habari jijini Dodoma.
Amesema Idadi ya watumishi watakaoajiliwa katika Kada za Ualimu ni 13,130 ambao watafundisha katika shule za Msingi a Sekondari.
Aidha, Waziri Kairuki ameeleza kuwa idadi ya watumishi watakoajiriwa katika kada za Afya ni 8,070 ambao watafanya kazi katika Hospitali za Halmashauri, Vituo vya Afya na Zahanati.
Waziri Kairuki amesema waombaji wanatakiwa kuomba ajira kuanzia leo April 12, hadi 25,2023 saa 5:59 usiku.
”Waombaji wote wanatakiwa kuwa na sifa za jumla kama zifuatazo awe mtanzania,awe na ukomo wa umri miaka 45 cheti Cha taaluma,cheti Cha kidato Cha sita na kitambulisho Cha NIDA.”amesema Waziri Kairuki
Waziri Kairuki amewataka waombaji waliowahi kutuma maombi ya ajira kupitia mfumo wa maombi ya ajira kuhuisha taarifa zao kwenye mfumo wa ajira kupitia kiunganishi ajira.tamisemi.go.tz kwa kutumia namba ya mtihani wa kidato cha nne na nywila au kuomba upya .
Amewataka waombaji wa ajira hizo kuwa tayari kufanyakazi kwenye Halmashauri na vituo watakavyopangiwa, kufanyakazi na mashirika au taasisi zilizoingia ubia na Serikali na baada ya kupangiwa kituo cha kazi hakutakuwa na nafasi ya kubadilishiwa kituo cha kazi
Aidha ametoa rai kwa waombaji wa ajira hizo kupeuka matapeli watakaowapigia simu na kuwataka kutoa fedha kwa ajili ya kupata ajira kwa kuwa ajira hizo ni bure, vigezo na masharti vitatumika katika kuwaajiri watumishi hao.
“Natoa rai kwa waombaji, mtu asije akapigiwa simu kuombwa fedha kwa ajili ya kupata ajira hizo, msiingie katika huo mtego kwa kuwa ikibainika hilo limejitikeza toeni taarifa kwa Mamlaka ili hatua stahiki zichukuliwe dhidi ya matapeli” amesisitiza Waziri Kairuki.