Home KITAIFA SERIKALI YAPOKEA MAJOKOFU 390 KWA AJILI YA KUHIFADHIA CHANJO

SERIKALI YAPOKEA MAJOKOFU 390 KWA AJILI YA KUHIFADHIA CHANJO

Serikali ya Tanzania yapokea majokofu ya kisasa 390 yenye thamani ya Sh Bilioni 3.27, kutoka kwa balozi wa Japan nchini, ambayo yatatumika  kuhifadhi chanjo.

 

Majokofu hayo tayari yameanza kusambazwa katika mikoa 13 nchini na yatatumika kuhifadhia chanjo za saratani ya mlango wa kizazi, Uviko-19 pamoja na chanjo za watoto..

Akipokea msaada huo jijini Dar es Salaam,Waziri wa Afya,Ummy Mwalimu amesema msaada huo umekuja wakati mwafaka, ambapo ili kufanikisha azma ya utunzaji chanjo majokofu 5,822 yanahitajika katika vituo vya chanjo nchini.

Ummy amesema hadi sasa serikali imenunua jumla ya majokofu mapya 2,012 na ununuzi wa majokofu mapya ya kisasa 3,810 unaendelea kwa kushirikiana na Shirika la UNICEF.

“Lengo la serikali kwasasa ni kuimarisha huduma za afya, ikiwemo huduma ya utoaji wa chanjo kwa watoto wenye uhitaji, hivyo majokofu haya yataboresha ubora wa kuhifadhi chanjo katika mnyororo wa baridi,” amesema.

Amesema serikali inalenga kuwa na majokofu ya kisasa ambayo yameunganishwa na vifaa maalum vya kupima joto la hali ya chanjo na kutuma taarifa kwa wahusika hata wanapokuwa mbali na kituo cha kuhifadhi chanjo.

Waziri Ummy amesema kipaumbele cha wizara hiyo kwa sasa ni utoaji wa chanjo hususan kwa watoto kutokana na tafiti mbalimbali kuonesha dola moja ya Marekani inayowekezwa katika chanjo huokoa dola 20 hadi 44 kwenye matibabu.

“Niwahakikishie kuwa kupitia msaada huu wa jokofu ya kuhifadhi chanjo tija yake itaonekana kwa kupunguza milipuko ya magonjwa yanayozuilika kwa chanjo kwa kufikia lengo la kuwachanja watoto kwa asilimia 95 kwa kila aina ya chanjo,”amesisitiza Ummy.

Waziri Ummy ametaja mikoa 13  itakayonufaika na majokofu hayo ni Arusha, Dar es Salaam, Lindi, Mtwara,  Shinyanga, Simiyu, Singida, Dodoma, Katavi, Rukwa, Tabora, Kigoma, Songwe na Zanzibar.

Previous articleWAWEKEZAJI WAHIMIZWA KUWEKEZA KATIKA SEKTA YA NISHATI YA UMEME NCHINI
Next articleWADAU WA MAENDELEO KUENDELEA KUSHIRIKIANA

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here