Home KITAIFA SERIKALI YAONDOA MAPINGAMIZI KESI YA BANDARI, MAHAKAMA KUU KUAMUA NI MKATABA AMA...

SERIKALI YAONDOA MAPINGAMIZI KESI YA BANDARI, MAHAKAMA KUU KUAMUA NI MKATABA AMA LAA

NA JOSEA SINKALA, MBEYA.

Upande wa wajibu maombi (Serikali) umeondoa mapingamizi yake manne iliyoyaweka hapo awali juu ya Kesi ya kikatiba ya kupinga mkataba wa Bandari iliyofunguliwa na wananchi mkoani Mbeya na kesi hiyo kuahirishwa hadi Julai 26, 2023 kwa ajili ya kuanza usikilizwaji.

Akizungumza mbele ya Mahakama kuu shauri hilo lilipokuja kwa ajili ya kusikilizwa, Wakili wa Serikali mkuu Mark Mulwambo kwa niaba ya wenzake ameiarifu mahakama kwamba upande wa waleta maombi na wajibu maombi wamekubaliana mambo kadhaa ambayo majaji watapaswa kujielekeza katika kuyatolea maamuzi na jambo moja ambalo pande hizo mbili hazijakubaliana.

Wakili Mulwambo amesema upande wao wajibu maombi wameyaondoa mapingamizi yao ya kisheria waliyoyaainisha juma lililopita juu ya shauri hilo hoja iliyokubaliwa na upande wa waleta maombi.

Akieleza makubaliano hayo mbele ya Mahakama Wakili wa waleta maombi wanaopinga mkataba wa bandari Mpale Mpoki amesema wamekubaliana majaji wajielekeze kwanza kubainisha ikiwa mkataba wa bandari unaoelezwa kusainiwa na kuridhiwa na Bunge ulikiuka misingi ya kisheria na ikiwa ni mkataba au laa.

Pia Wakili Mpale Mpoki amesema pia wamekubaliana uamuzi utolewe ikiwa umma ulishirikishwa ipasavyo kutoa maoni yao hata kukubaliwa kwa mkataba huo na ikiwa vifungu mbalimbali vilikiukwa kikiwemo kifungu namba 2 (4) a, kifungu namba 5 (1) na 6 (2) vyote vya mikataba ibara namba 1 ya katiba ya Tanzania ya mwaka 1977.

Pia Mahakama itakuwa na wajibu wa kuangalia ikiwa wahusika kwenye mkataba walikuwa na nguvu kisheria kuingia kwenye mkataba wa bandari.

Hata hivyo Jaji Dustan Ndunguru kwa niaba ya jopo la majaji wenzake wawili wa Mahakama kuu ya Tanzania Kanda ya Mbeya ameahirisha kesi hiyo namba 05/2023 hadi jumatano hii ambapo shauri litaanza kusikilizwa rasmi baada ya mapingamizi ya Serikali kuondolewa.

Ikumbukwe waleta maombi kwenye shauri hilo ni Alfonce Lusako, wakili Emanueli Chengula, Raphael Ngonde na Frank Nyalusi wakiwakilishwa mahakamani na mawakili Boniface Mwabukusi, Wakili Mpoki, Phillip Mwakilima na Livino Ngalimitumba huku wajibu maombi yaani Serikali kwa niaba ya wateja wao ikiongozwa na Wakili wa Serikali mkuu Mark Mulwambo, Wakili wa Serikali mkuu Edson Mweyunge, Wakili wa Serikali mwandamizi Alice Mtulo na Wakili wa Serikali Edwin Wabiro.

Kesi hii ya kikatiba kuhusu kupingwa mkataba wa bandari imeonekana kufuatiliwa kwa ukaribu na makundi mbalimbali wakiwemo wanasiasa na viongozi wa dini ndani na nje ya mkoa wa Mbeya.

Previous articleDODOMA JIJI FC WAENDELE KIJIFUA MKOANI IRINGA
Next articleDEREVA BAJAJI MBARONI KWA TUHUMA ZA KUMUUA MGAMBO KWA KISU KIKATILI _ MAGAZETINI LEO JUMATANO JULAI 26/2023

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here