Serikali imesema itazichukulia hatua shule zitakazoendelea kutoa huduma ya bweni kwa Watoto chini ya darasa la Tano
Kauli ya Serikali imetolewa na Naibu Waziri wa Elimu ,Sayansi na Teknolojia Omary Kipanga juni 21, 2023 Bungeni jijini Dodoma wakati Akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Judith Kapinga aliyetaka kujua mkakati wa serikali kudhibiti Watoto chini ya umri wa miaka saba kusomo Shule za Bweni.
Kipanga amesema Waraka wa Elimu Na 2 wa Mwaka 2023 unawaelekeza wamiliki wa shule wasiokuwa na kibali Maalumu cha kutoa huduma ya bweni kwa wanafunzi waliochini ya Darasa la Tano wasiendelee kutoa huduma hiyo.
Aidha, kwa kushirikiana na wadau wa elimu, Wizara inakamilisha kuandaa vigezo vitakavyotumiwa na Kamishna wa Elimu katika kutoa kibali Maalumu.
‘’ Napenda kulijulisha Bunge lako tukufu kuwa Serikali itaendelea kudhibiti tatizo la Watoto chini ya darasa la Tano kusoma shule za bweni kwa kuhakikisha kuwa inafanya ufuatiliaji wa mara kwa mara na shule itakayobainika kukiuka maelekezo hayo itachukuliwa hatua za kinidhamu, na kisheria ikiwemo kufutiwa usajiLI,’’.amesema Kipanga.