Serikali kupitia wizara ya Maji imesema wananchi wa vijiji 11 vya Msangano, Nkala, Makamba, Naming’ongo, Yala, Ipata, Ntinga, Chindi, Isanga, Kakozi na Mlonga katika tarafa za Kamsamba na Ndalambo wanakwenda kukombolewa na kadhia ya kukosa huduma ya maji safi kwani Serikali inaendelea kujenga miradi kadhaa ya maji na itamalizika hivi karibuni.
Hayo ni kufuatia swali la Mbunge Condester Michael Sichalwe Bungeni jijini Dodoma alipotaka kujua ni lini Serikali itamaliza kero ya maji jimboni kwake ambapo wizara ya Maji imejibu.
“Mhe. Spika Serikali inatambua adha ya Maji wanayopata wananchi wa wilaya ya Momba na tayari hatua zimeanza kuchukuliwa. Katika mwaka wa fedha 2022/2023 miradi ya Maji ya Naming’ongo-Msangano, Isanga-Kakozi na Tindingoma Mlomba inaendelea kutekelezwa”, Waziri wa Maji Mhe. Juma Aweso (hayupo pichani), akijibu swali la Condester Sichalwe (Mundi) Mbunge wa Momba mkoani Songwe.
“Katika mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali itaendelea kutekeleza miradi ya Maji kupitia chanzo cha Maji cha mto Momba ili kuhakikisha wanachi katika vijiji vilivyobaki wilayani Momba wanapata huduma ya maji safi na salama nanyenye kutosheleza”, Waziri wa Maji Mhe. Juma Aweso.